DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Marcio Maximo, ametangazwa rasmi kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Kinondoni Municipal Council (KMC FC) kwa mkataba wa mwaka mmoja, kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Maximo, ambaye anatokea nchini Brazil, aliwahi pia kuifundisha klabu ya Yanga miaka 10 iliyopita, anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya soka la Tanzania, hasa alipokuwa na Taifa Stars kati ya mwaka 2006 hadi 2010. Amewasili nchini akiwa ameambatana na msaidizi wake, ambaye bado hajatajwa rasmi.
Akizungumza mara baada ya kutambulishwa, Maximo alisema amejiunga na KMC kwa sababu ameridhishwa na mipango ya viongozi wa klabu hiyo, akiahidi kuipeleka timu hiyo kwenye mafanikio makubwa msimu huu.
“Malengo yangu ni kuhakikisha KMC inafanya vizuri msimu ujao. Ninaamini kwa ushirikiano wa mashabiki wa Kinondoni, tutafanikisha malengo yetu,” alisema Maximo.
Kocha huyo aliongeza kuwa tayari amepitia ripoti ya kocha aliyemtangulia, Kally Ongala, na baadhi ya mapendekezo yake ya usajili yamezingatiwa katika maandalizi ya kikosi kipya.
Kwa upande wake, Msemaji wa KMC, Khalid Chuku Chuku, alisema klabu hiyo imeamua kumleta Maximo kutokana na uzoefu na uwezo mkubwa alionao.
“Tumemchukua Maximo kwa sababu ya rekodi na maono yake ya kisoka. Tunataka KMC ipate nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa, na tunaamini anaweza kutufikisha huko,” alisema Chuku Chuku.
Aliongeza kuwa tayari wamesajili wachezaji wanne wapya na kuwaaga wachezaji nane waliomaliza mikataba yao. KMC inatarajia kuanza kuwatambulisha wachezaji wapya hivi karibuni kabla ya kuelekea Visiwani Zanzibar wiki ijayo kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya wiki nne.
The post Maximo arejea Ligi Kuu first appeared on SpotiLEO.