…………
Na Mwandishi Wetu
Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasher Mkoa wa Dar es salaam imeandaa Kambi ya bure ya Afya na Macho kwa siku tatu kuanzia Ijumaa hadi jumapili ya wiki hii katika viwanja vya Mnazi Mmoja yaliyopewa jina la mafunzo ya Imam Hussain (a.s) ambaye alifariki huko Karbala nchini Iraq miaka 1400 iliyopita.
Kambi hiyo ya bure ni mwendelezo wa jitihada za jumuiya hiyo katika utoaji huduma kwa jamii bila malipo na katika siku hiyo kutatolewa huduma za afya na macho maarufu kama “Mafunzo ya Imam Hussain” inatarajiwa kufanyika kuanzia saa 2: 00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Mkoa wa Dar es salaam Alhadji Mohamedraza Dewji amesema kuwa kambi hiyo ambayo mwaka jana ilihudumia maelfu ya wananchi, inaleta pamoja wataalamu wa afya, taasisi mbalimbali, na mashirika ya tiba kutoka ndani ya Tanzania, katika juhudi ya pamoja ya kuwafikia wale wasio na uwezo wa kupata huduma hizi kwa urahisi.
Pia, Mwenyekiti huyo amesema kuwa mbali na utolewaji wa huduma hizo katika kambi hiyo ya siku tatu pia kutatolewa Miwani na Dawa bure, pamoja na uchunguzi wa mtoto wa jicho (cataract.)
Aidha, Mwenyekiti huyo amesema kuwa kutatolewa bure kwa Vipimo vya sukari, shinikizo la damu, uzito na urefu (BMI) na elimu juu ya ugonjwa uliosahaulika wa afya ya akili, Uchunguzi wa saratani ya matiti na shingo ya kizazi kwa kina mama kwa ushirikiano na taasisi ya cancer ya Ocean Road.
Vile vile, Mohamedraza amesema kuwa kutakuwa na uchangiaji wa Damu kwa kushirikiana na Taasisi ya Damu Salama huduma hizo zitatolewa bila gharama yoyote, na zinalenga kuwahudumia wananchi wote, bila kujali Dini, Kabila, au hali ya maisha” amesema Alhadji Mohamedraza.
Alhadji Mohamedraza, amesema kuwa uwazishwaji wa utolewaji wa huduma hizo bure inatokana na kupatiwa jina kutoka Karbala, Jina la Kambi hiyo linatokana na Imam Hussain (a.s), mjukuu wa Mtume Muhammad (s), ambaye alisimama kwa misingi ya haki, huruma na huduma kwa binadamu katika tukio mashuhuri la Karbala.
“waanzilishi wa kambi hiyo wanasema kuwa lengo ni kugeuza mafunzo ya Karbala kuwa vitendo vya huruma vinavyogusa maisha ya watu, hasa walioko pembezoni ” amesema Mwenyekiti Mohamedraza.
Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya washiriki wa miaka iliyopita, kambi hii imekuwa si tu chanzo cha afya bora kwa wananchi, bali pia ni darasa la maadili, likiunganisha watu wa makundi mbalimbali kwa msingi wa utu na huduma.
Ushiriki wa Jamii ya Waislamu wa Shia katika kambi hiyo inayoandaliwa kila mwaka na jamii ya Waislamu wa Shia wa Mkoa wa Dar es salaam maarufu kama Khoja Shia Ithna-Asheri Jamaat kama wafuasi wa Ahlulbayt familia ya Mtume Muhammad (s) jamii hii hujielekeza katika matendo ya kusaidia waliodhulumiwa, wagonjwa, na wahitaji, wakisisitiza kuwa dini ya kweli hujidhihirisha katika matendo mema.
Kwa mujibu wa jumuiya hiyo Mkoa wa Dar es salaam, hii ni njia ya kuhuisha urithi wa Imam Hussain (a.s), lakini kwa watu wa kawaida, ni fursa ya kupata huduma muhimu za afya kwa heshima, kwa huruma, na bila Gharama.