Farida Mangube, Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, ametoa wito kwa wakazi wa mikoa ya Pwani, Dar es salaam, Tanga na Morogoro kujitokeza kwa wingi kutembelea Maonesho ya 32 ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane), yatakayofanyika kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2025 katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, mjini Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari Mhe. Malima amesema maonesho hayo yatakuwa jukwaa muhimu kwa wananchi kujionea teknolojia za kisasa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, kujifunza mbinu bora za uzalishaji na kuunganishwa na fursa za masoko, mitaji na elimu ya kitaalamu.
“Tunawahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho haya. Ni fursa ya kipekee kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali kujifunza, kuonesha mafanikio na kushiriki katika majadiliano ya kitaalamu kuhusu maendeleo ya sekta ya kilimo,” amesema RC Malima.
Kwa mujibu wa RC Malima, maandalizi ya maonesho hayo yamefikia zaidi ya asilimia 98, huku Serikali ikitekeleza maboresho mbalimbali ikiwemo uchimbaji wa visima vya maji ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa washiriki na wageni.
Maonesho ya mwaka huu pia yataambatana na jukwaa maalum la B2B (Business to Business) litakalofanyika kuanzia Agosti 2 hadi 7, ambapo wataalamu kutoka taasisi za ndani na kimataifa watatoa mada juu ya maendeleo ya kisekta, fursa za uwekezaji, na teknolojia mpya.
Amesema mgeni rasmi wa siku ya uzinduzi anatarajiwa Kuwa Waziri Mkuu Mstafu Mhe, Mizengo Pinda, huku kilele cha maonesho tarehe 8 Agosti kikitarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, mabalozi, wawakilishi wa taasisi za maendeleo na wananchi kutoka mikoa yote ya Kanda ya Mashariki.
Mbali na elimu na maonesho ya bidhaa, maonesho ya mwaka huu pia yatakuwa na burudani za kiutamaduni, michezo na matukio ya kijamii ili kuvutia wananchi wa rika na makundi yote.