
………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo limefanikiwa kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa makundi mbalimbali huku kampeni shirikishi ya kutoa elimu kwa jamii zikitajwa kuwa sababu.
Akizungumza wakati wa kupokea spika 10 zinazotembea (movable speakers) kutoka Shirika la Railway Children Village Society (SOS), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa, amesema Jeshi la Polisi limefanikiwa kupunguza uhalifu utokanao na ukatili wa kijinsia kwa asilimia 11.46 ikilinganishwa na mwaka jana kwa kipindi cha miezi saba kuanzia Januari.
“Mwaka jana (2024) yaliripotiwa makosa ya kubaka 155 na mwaka huu yameripotiwa makosa 135, makosa 19 yamepungua. Makosa ya kuzini na maarimu mwaka huu yameripotiwa matukio 3, mwaka jana yaliripotiwa matukio 5,” ameeleza Kamanda Mutafungwa.
Aidha, Kamanda Mutafungwa amesema makosa mengine yaliyopungua ni pamoja na wizi wa mtoto, ambapo mwaka huu yameripotiwa matukio 2 ikilinganishwa na matukio 5 mwaka jana. Vilevile, matukio ya kutupa mtoto yamepungua kutoka matukio 12 mwaka jana hadi matukio 7 mwaka huu, matukio ya kulawiti yamepungua kutoka matukio 45 mwaka jana hadi hadi matukio 41 mwaka huu.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Miradi wa shirika la SOS, Bi. Elizabeth Swai, amesema kuwa shirika lao linaloshughulika na watoto waliopoteza malezi na walio katika hatari ya kupoteza malezi, limetoa msaada wa spika 10 zinazotembea, vibao vyenye jumbe mbalimbali, na mabango manne, vyote vikiwa na thamani ya Shilingi milioni 18. Lengo kuu la msaada huu ni kuendeleza elimu kwa jamii na familia.
“Tunaamini kuwa vifaa hivi tulivyotoa vitasaidia elimu kuendelea kutolewa kwenye jamii na watoto wataendelea kubaki salama. Tunaamini katika usalama ndiko tunakopata amani ya kitaifa na kwenye ngazi ya familia ambayo itasaidia mtoto aweze kufikia malengo,” alisema Bi. Swai.
Naye Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza, Godlave Landala, amesema kampeni iliyozinduliwa na Kamanda Mutafungwa imeleta mafanikio makubwa kwani imesaidia kuibua matukio mengi ya ukatili yaliyokuwa yanafichwa na mengi yametafutiwa ufumbuzi.
Mafanikio haya ni matokeo ya kampeni iliyofanyika kwa kipindi cha mwezi mmoja, iliyozinduliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, tarehe 22 Aprili 2025, katika Kata ya Kayenze, Wilaya ya Ilemela, na kutembelea zaidi ya kata 20 ikiwa na Kauli mbinu “Mwanza salama, Mtoto salama”