Sinzo Khamis Mgeja, mtoto  wa Mwanasiasa maarufu nchini, Comrade Khamis Mgeja ni mmoja wa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walioteuliwa na Kamati Kuu (CC), kuwania Ubunge wa Viti Maalum kupitia (Umoja wa Wanawake (UWT), kundi la Wazazi Bara.
Mgeja amepata kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga na Mjumbe wa NEC taifa na kuzitumikia nafasi hizo kwa mafanikio makubwa ambaye kwa sasa yuko nchini India kwa ajili ya matibabu ya mguu.
Akizungumza na mwanahabari wetu baada ya uteuzi huo, Sinzo ambaye kitaaluma ni Mwalimu, amesema amepokea kwa furaha uamuzi huo kwani chama kimemuamini naye yuko tayari kukitumikia kwa moyo na uwezo wake wote endapo wajumbe watampa ridhaa.
Mwalimu Sinzo amesema endapo akipewa ridhaa ya kuchaguliwa na wajumbe ni wakati muafaka wa kushirikiana na wazazi wenzake na chama chake cha CCM  kutatua changamoto zinazowakabili wazazi.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na masuala ya uchumi na maendeleo na kuporomoka kwa maadili kwenye baadhi ya jamii hasa vijana na mengineyo.
Kada huyo ambaye ni  Mjumbe wa Kamati Ndogo ya Elimu na Mazingira Wilaya ya Kisarawe, alisema kupitia kauli mbiu ya ‘Kazi na Utu Tunasongambele endapo atafanikiwa kupata nafasi hiyo, atachapa kazi kwa kushirikiana na wenzake kuhakikisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafikisha malengo ya kuipeleka Tanzania kwenye Dira ya Maendeleo ya miaka 50 ijayo.
“Ninakishushukuru sana chama changu kwa kuniamini na kuniteua kuwa miongoni mwa wagombea wa nafasi za  ubunge wa Viti Maalum na nina imani nikipata ridhaa nitaitendea haki nafasi yangu,” alisema Sinzo Mgeja.
Kamati Kuu (CC) ya CCM, imekamilisha kazi ya kufanya uteuzi wa awali kwa wagombea ubunge wa majimbo, viti maalum na ujumbe wa baraza la wawakilishi.
Katibu wa Itikadi na Uenezi na Mafunzo NEC, Amosi Makalla alikiri kuwa uteuzi huo ulikuwa mgumu kutokana na idadi kubwa ya wagombea waliojitokeza kuliko wakati mwingine wowote wa chama hicho.