Songea_Ruvuma.
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) imeanza hatua za usambazaji wa mita za maji za mfumo wa luku kwa baadhi ya taasisi, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuboresha huduma zake kwa wateja na utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa mwaka jana.
Akizungumza Meneja wa Huduma kwa Wateja kutoka SOUWASA Jumanne Gayo, amesema kuwa mamlaka hiyo imepokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau kuhusu uhitaji wa mita hizo, na tayari mita 365 zimeshafungwa katika maeneo mbalimbali kwa wateja wa Taasisi, Biashara na Binafsi wenye matumizi makubwa.
“Huu ni mchakato unaoendelea, na tumeshaanza kufunga mita kwawateja kadhaa kwa hatua za awali kutokana na mita hizo kugharimu fedha nyingi. Baada ya kujiridhisha na ufanisi wake, tutatoa tangazo rasmi kwa wateja wote kuhusiana na upatikanaji wa huduma hii,” alisema Gayo.
Ameongeza kuwa lengo kuu ni kujibu kilio cha muda mrefu cha wateja waliokuwa wakitaka kubadilishiwa mita za kawaida kuwa mita za mfumo wa luku, ambazo ni rahisi kudhibiti matumizi na kupunguza migogoro ya bili.
Kwa upande wake, Mhandisi Vicent Bahemana kutoka SOUWASA ameeleza kuwa utaratibu wa usomaji wa mita unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wateja na wasomaji wa mita. Alisisitiza kuwa jukumu la SOUWASA linaishia kwenye mita, na maji yanapoingia ndani ya nyumba ni jukumu la mteja kuhakikisha usalama na matengenezo ya vifaa.
“Mara ya kwanza mteja anapounganishwa na huduma vifaa vinatolewa bure baada ya kulipia gharamaza kuunganishiwahuduma, lakini ukitokea uharibifu mteja atapaswa kugharamia matengenezo au uingizwaji wa kifaa hicho,” alisema Bahemana.
Naye mmoja wa wasomaji dira wa mamlaka hiyo Amiri Chata amesema elimu kwa wananchi inaendelea kutolewa, ingawa changamoto kubwa imekuwa ni ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wateja.
“Wakati wa usomaji dira, tunawashirikisha wateja ili kuhakikisha uwazi. Hata hivyo, wapo wateja wanaotoa ushirikiano mdogo au majibu yasiyo rafiki ,” alieleza.
Aliongeza kuwa baada ya kusoma mita, wateja hupokea ujumbe wa taarifa ya matumizi, na kati ya tarehe 8 hadi 16 ya kila mwezi, SOUWASA hufanya uhakiki wa matumizi ili kubaini tofauti na kuchukua hatua stahiki, ikiwemo kuwasiliana moja kwa moja na wateja walioonekana kutumia maji kupita kiasi au kidogo.
Mchakato huu wa maboresho unatarajiwa kuongeza uwazi, usimamizi bora wa matumizi ya maji na kuleta huduma ya kisasa kwa wateja wa SOUWASA, Mamlaka imetoa wito kwa wateja kuwa na subira huku taratibu zikiendelea kukamilishwa.
Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Songea SOUWASA, inaendelea na utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa mwaka jana, zoezi la kufunga mita za malipo ya kabla au luku kwa wateja wake, hii ni sehemu ya uboreshaji wa huduma ya usambazaji wa huduma zake kwa wateja ambapo tayari utekelezaji unaendelea na wananchi wawe wavumilivu wakati jitihada zakuwafikia wateja wote zinaendelea.