DAR ES SALAAM: Baada ya kufikia watoto zaidi ya milioni 48 barani Afrika kupitia vipindi vyake vya Akili and Me na Ubongo Kids, shirika la Ubongo limezindua rasmi Msimu wa Tano wa kipindi maarufu cha watoto, Akili and Me, ukiwa na sura mpya, uhuishaji wa kisasa, na msisitizo mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kihisia kwa watoto wadogo.
Ubongo, linalotambulika kama shirika kinara barani Afrika katika kuunganisha elimu na burudani (edutainment), limekuwa mstari wa mbele katika kubadilisha namna watoto wanavyopokea elimu, kwa kutumia mbinu za kisasa zinazojumuisha muziki, hadithi, na vipengele vya kushirikisha watoto moja kwa moja.
Msimu huu mpya wa Akili and Me umejikita katika mafunzo ya kijamii na kihisia (Social-Emotional Learning – SEL), ukiwapatia watoto maarifa ya kutambua, kuelewa, na kueleza hisia zao kwa njia chanya, hatua inayosaidia kujenga ujasiri, huruma, na ustahimilivu wa kihisia mapema katika maisha yao.
“Kupitia Msimu wa Tano, tulitaka kwenda zaidi ya ABC na 123 kwa kuangazia kitu cha msingi zaidi—kuwasaidia watoto kuelewa na kueleza hisia zao,” amesema Tamala Maerere-Kateka, Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano ya Kimkakati wa Ubongo. “Tunaamini kuwa watoto wanapojifunza jinsi ya kushughulikia hisia zao, hujijengea ujasiri na ustahimilivu unaohitajika kufanikiwa shuleni na maishani.”
Kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu ya uhuishaji, wahusika wa kipindi wamebuniwa upya kwa rangi zenye mvuto na sura zenye uhalisia zaidi, jambo linalolifanya somo kuwa la kuvutia na kuwavutia watoto zaidi. Hii ni hatua ya kuongeza ushirikiano kati ya watoto na maudhui ya kipindi pamoja na wazazi au walezi wao.
Ubongo pia imezindua Akili and Me Games kupitia programu ya Ubongo Playroom, ikiwa ni jukwaa la kisasa la kujifunzia linalojumuisha video za elimu, hadithi za sauti, vitabu vya kidijitali, na michezo ya kielimu. Programu hii inalenga kuongeza ushiriki wa watoto kwa njia ya kucheza, kujifunza, na kuchunguza kwa uhuru zaidi. “Tunafahamu kuwa watoto hujifunza vizuri zaidi kupitia michezo,” ameongeza Maerere-Kateka.
Kwa zaidi ya miaka kumi ya mafanikio, Akili and Me kimeendelea kuwa darasa la kwanza kwa mtoto, rafiki wa karibu, na lango la elimu ya maisha. Kupitia msimu huu mpya, Ubongo inaendeleza dhamira yake ya kuhakikisha kila mtoto barani Afrika anapata elimu ya awali iliyo na maana, jumuishi, na inayobadilisha maisha. “Hisia kubwa zinaweza kuwa nzito kwa watoto wadogo, lakini wanapopata maneno na mbinu za kujieleza, hujenga ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha,” amehitimisha Maerere-Kateka.
Kwa maelezo zaidi kuhusu msimu mpya wa Akili and Me, tembelea: www.akiliandme.com
The post Sura mpya kwa akili and Me first appeared on SpotiLEO.