

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema hakubaliani na kauli ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwamba hakuna njaa huko Gaza. Akiwa kwenye uwanja wake wa gofu nchini Scotland, Trump alisema, “Kwa kuangalia kwenye televisheni, naona watoto wanaonekana wenye njaa.”
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, aliyeonana na Trump, alielezea hali ya kibinadamu Gaza kuwa “janga kamili” na “hali ya kukatisha tamaa.” Alisema wananchi wa Uingereza wanahuzunishwa na picha wanazoona, na alisisitiza umuhimu wa kusitisha vita.
Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani zimekosoa Israel kwa kuzuilia misaada muhimu ya kibinadamu huku njaa ikizidi kuenea Gaza. Starmer ametangaza kuwa Uingereza itashiriki katika operesheni za angani za kutoa misaada pamoja na Jordan, baada ya Israel kulegeza masharti kwa muda.
Wakati huo huo, mashirika ya haki za binadamu yameeleza wasiwasi mkubwa juu ya taasisi ya GHF, wakiiita “njama ya kisiasa yenye madhara.” Takriban Wapalestina 900 wameuawa hivi karibuni wakijaribu kupata chakula karibu na vituo vya GHF, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV — usisahau ku-like, ku-comment na ku-subscribe ili uendelee kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.