Na WMJJWM- Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju amepongeza uongozi wa Mfuko wa Abbot Fund kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya watoto wenye mahitaji maalum.
Wakili Mpanju amesema hayo Julai 30, 2025, Jijini Dodoma baada ujumbe wa Mfuko huo kutembelea Makao ya Taifa ya Watoto yaliyopo Kikombo.
Wakili Mpanju amesema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, inatoa pongezi na shukrani kwa uongozi wa Mfuko wa Abbot Fund kwa kuendelea kushirikiana ili kuwezesha kustawisha maisha ya watoto wanaolelewa katika Makao ya Taifa na jamii kwa ujumla.
Katika ziara hiyo pia Wakili Mpanju amepokea vifaa mbalimbali kwa ajili ya watoto kujifunzia kutoka mfuko wa Abbot Fund vikiwemo komputa, madaftari na mavazi.
Aidha Wakili Mpanju ameongoza ujumbe huo kutembelea mradi wa kilimo, ufugaji wa samaki na karakana ya ushonaji ambapo watoto hao upata ujuzi ili waweze kujiajiri mara wanapotoka katika Makao hayo.
Akizungumza katika uwasilishaji wa vifaa hivyo Makamu Mkurugenzi wa Mfuko huo Julia Gin amesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuhakikisha watoto wanaolelewa katika makao wanapata huduma stahiki na stadi za maisha.