………
Na Mwandishi Maalum, Namtumbo
WAKULIMA wa zao la Tumbaku katika kijiji cha MkongoNakawale Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma, wamepongeza mpango wa Serikali wa kutoa mbolea za ruzulu iliyosaidia kuongeza uzalishaji na kujikwamua na umaskini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema,kupitia mbolea za ruzuku wamelima tumbaku yenye ubora iliyowezesha kupata soko la uhakika na bei nzuri ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo wanunuzi walikwenda mashambani kununua Tumbaku kwa bei ndogo isiyolingana na gharama halisi ya uzalishaji.
Meneja wa Chama cha Msingi MkongoNakawale Micheal Komba alisema,tangu Serikali ilipoanza kutoa mbolea za ruzuku kwenye zao la Tumbaku wamekuwa na maisha mazuri kwa kuwa wanazalisha mazao yenye ubora mkubwa yanayowaingizia fedha nyingi tofauti na miaka ya nyuma ambapo pembejeo ziliuzwa kwa bei kubwa.
“tunaishukuru Serikali kupitia Wizara ya kilimo na Ushirika kwa kutoa pembejeo hususani mbolea za ruzuku,zimesaidia sana sisi wakulima kupata kwa urahisi na jambo lililo changia sana uzalishaji kwa wakulima wanaohudumiwa na Chama chetu”alisema Komba.
Alisema,awali vyama vingi vya ushirika vilizalisha madeni makubwa kutoka kwenye taasisi za fedha ambayo hayakulipika,lakini tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani imeanza kulipa madeni hayo na vyama kuanza kukopeshwa pembejeo na fedha kwa ajili ya wanachama wake.
Aidha alisema,katika kipindi cha miaka miwili uzalishaji wa tumbaku umeongezeka kutoka wastani wa tani 100 zenye thamani ya Sh.milioni 355 mwaka 2024 hadi kufikia tani 206 zenye thamani ya Sh.milioni 914 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 100.
Alisema,mafanikio hayo yamechangiwa baada ya Serikali kusimamia sekta ya kilimo na ushirika kwa kuwa bei ya mbolea aina ya NPK na UREA inayotumika kwenye zao hilo kupungua kutoka Sh.170 hadi Sh.145,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 25.
Mkulima wa tumbaku katika kijiji cha MkongoNakawale Edwin Kawonga alisema,zao la tumbaku kwa sasa lina mchango mkubwa kiuchumi kwa mkulia mmoja mmoja,wilaya ya Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma hasa baada ya Serikali kusimamia kwa karibu bei ya zao hilo na mazao mengine yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
“hapo awali tumbaku ya mvuke ilikuwa hailimwi na wanachama wa chama hiki tulikuwa tunalima tumbaku ya moshi ambayo bei zake ziko chini,lakini baada ya Serikali kuhamasisha kulima tumbaku ya mvuke watu wengi wamehamasika kutokana na bei kuwa kubwa,sisi kama wakulima tunafurahia na tunaiomba Serikali iendelee kutuhamasisha kulima zao hili”alisema Kawonga.
Alisema,miaka ya nyuma tumbaku ya mvuke daraja la kwanza iliuzwa kati ya dola 1.5 hadi 2,lakini katika kipindi cha miaka mitatu bei imeongezeka kutoka dola 2 hadi dola 3.20 kwa kilo moja.
Mkulima mwingine Issa Ndauka alisema,katika msimu wa mwaka huu amelima ekari mbili zilizomungizia zaidi ya Sh.milioni 3 baada ya kuuza tumbaku kwa njia ya stakabadhi ghalani.
Kwa upande wake Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya Namtumbo Shaban Seleman,amewataka wakulima kuanza kulima tumbaku ya mvuke ambayo bei yake ni kubwa ikilinganisha na tumbaku ya moshi katika msimu wa kilimo 2025/2026.
Seleman,amewahimiza wakulima kujiozesha na kujiunga na kwenye ushirika ili waweze kupata pembejeo kwa urahisi zitakaochochea kuongezeka kwa uzalishaji mashambani na kujikomboa na umaskini.
“mzao la tumbaku ya mvuke kweli linalipa sana,mwaka huu imeuzwa kwa dola 3.32 ikilinganisha na tumbaku ya moshi iliyouzwa kwa dola 2,nawaasa wakulima wajitokeze kwa wingi kwani maendeleo yanakuja kwa watu kufanya kazi,ili tupate maendeleo ni lazima tujikite kwenye kufanya kazi tupate fedha ili tufanye maendeleo katika wilaya ya Namtumbo na nchi kwa ujumla”alisema Seleman.