Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amekutana na vijana viongozi kutoka Tanzania wanaoshiriki katika mageuzi ya mifumo ya chakula kupitia mradi wa Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) chini ya kampeni ya Vijana4Food.
Mazungumzo hayo yamefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Mfumo wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (UNFSS+4) uliofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 27 hadi 29 Julai 2025 jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Kupitia mkutano huo, Waziri Kombo amewapongeza vijana hao kwa kuwa sehemu ya mabadiliko makubwa katika sekta ya chakula, akiwataka kutumia fursa hiyo kuleta mawazo bunifu na kuongoza kwa vitendo mageuzi ya mifumo ya chakula yenye lishe bora, salama na endelevu nchini Tanzania.
“Nyinyi ni sauti muhimu ya vijana wa Tanzania kwenye majukwaa haya ya kimataifa. Mtumieni nafasi hii kwa manufaa ya Taifa na kuchangia maendeleo ya mifumo endelevu ya chakula,” amesema Mhe. Kombo.
Mradi wa GAIN unalenga kuwawezesha vijana kushiriki kwa dhati katika sera, mikakati na utekelezaji wa mabadiliko ya mifumo ya chakula kwa mustakabali bora wa kizazi cha sasa na kijacho.