
WATAFITI wa Kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wameitaja Mbegu ya Zabibu ijulikanayo kama Makutupora nyekundu (Makutupora Red) kuwa ni Mbegu ambayo imethibitika kuwa na sifa za kipekee Duniani.
Hayo yamesemwa Leo Julai 30, 2025 na Mtafiti Mwandamizi kutoka kituo cha TARI Makutupora Bi. Felista Mpore wakati akizungumza katika Moja ya kituo cha Radio Jijini Dodoma ambapo ametaja sifa za Mbegu hiyo inayolimwa zaidi hapa nchini kuwa ni uwezo wa kutoa kiwango kikubwa cha sukari ambacho ni kigezo kinachozingatiwa katika usindikaji.
Bi. Felista ametaja sifa zingine kuwa ni uwezo wa kustahimili magonjwa, kuhimili ukame kutoa Mavuno mengi na kuwa na rangi nyingi.
Kwa mujibu wa Mtafiti huyo, Watafiti Kutoka nchi mbalimbali kwa nyakati tofauti walichukua vinasamba kulinganisha na Mbegu zingine Duniani wakarudi na majibu kuwa Mbegu hiyo inayolimwa ina sifa za kipekee.
Aidha Bi Felista amewashauri Wakulima kujikita katika kuongeza thamani zao hilo ili kujipatia tija suala ambalo amesema TARI inatoa mafunzo kwa Wadau wa Kilimo na kuelekea msimu wa Maonesho ya Kilimo maarufu Nanenane wataendelea na kutoa elimu katika viwanja mbalimbali ikiwemo kitaifa Nzuguni Jijini Dodoma.
