NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
Kampuni ya kimataifa ya FUCHS Lubricants Tanzania Limited imezindua rasmi oili mpya yenye ubora wa hali ya juu kwa ajili ya injini za pikipiki na bajaji, maarufu kama boda boda, iitwayo TITAN MAX 4T SL 20W50.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 30, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla hiyo, Meneja wa Fedha wa Kampuni hiyo, Bw. Taalib Shariff amesema kuwa kwa muda mrefu FUCHS haikuwa sokoni na oili mahsusi za pikipiki, hali iliyosababisha changamoto kwa madereva wengi.
Amesema kampuni ilichukua muda kufanya tafiti za kisayansi kwa kuzingatia mazingira ya kijiografia ya Tanzania ikiwemo joto, baridi na vumbi pamoja na aina ya mafuta yanayotumika, ili kuhakikisha inazalisha bidhaa bora inayokidhi mahitaji ya soko.
“TITAN MAX 4T SL 20W50 imetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa ili kulinda injini, kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za matengenezo. Tunataka madereva wa boda boda na bajaji wawe na uhakika wa kipato bila usumbufu wa injini kuharibika mara kwa mara.” amesema
Aidha amesema kuwa Oili hii yenye ubora wa viwango vya kimataifa vya API SL na SAE 20W50 inatoa huduma muhimu kwenye injini ikiwemo, Kulainisha sehemu zote zenye msuguano, Kuzuia kutu, Kusafisha injini na Kuipoza injini.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mauzo wa Kanda Bw. Albert Ng’ingo amesema kuwa kwa kutumia TITAN MAX 4T SL 20W50, madereva wanapata uhakika wa kuendesha vyombo vyao kwa muda mrefu bila matengenezo ya mara kwa mara, hivyo kuongeza kipato na kupunguza hasara zinazotokana na kuvunjika kwa injini katikati ya shughuli.
“Tunawaalika madereva wote wa pikipiki na bajaji kutumia oili hii ili kufanikisha shughuli zao za kila siku na kuongeza mapato. FUCHS tumejipanga kuleta suluhisho endelevu katika sekta ya usafirishaji,” ameongeza Bw. Shariff.