AALBORG: MCHEZAJI chipukizi wa Tanzania, Kelvin John, ameendelea kung’ara katika anga za kimataifa baada ya kutangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Julai katika klabu yake ya Aalborg inayoshiriki Ligi ya Denmark.
Kelvin, ambaye aliwahi kuonesha uwezo mkubwa akiwa na kikosi cha Serengeti Boys na baadaye Taifa Stars, ametwaa tuzo hiyo kupitia kura za mashabiki zilizoratibiwa na wadhamini wa klabu hiyo, Faxe Kondi.
Kupitia kura hizo, mashabiki walimchagua kuwa mchezaji bora zaidi wa mwezi kutokana na mchango wake mkubwa uwanjani, hasa kasi, maarifa ya kiufundi na uwezo wake wa kufumania nyavu.
Katika taarifa iliyotolewa na klabu hiyo kupitia mitandao ya kijamii, iliandikwa: “
“Kelvin John ametangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi wa klabu ya AaB! Mashabiki kupitia upigaji kura wa Faxe Kondi wamemchagua Kelvin John kama mchezaji bora wa mwezi Julai.”
Tuzo hiyo ni uthibitisho wa ubora wa mshambuliaji huyo kijana anayezidi kuimarika barani Ulaya, na ni habari njema kwa watanzania wanaomfuatilia kwa karibu wakitumaini kuwa atakuwa sehemu ya mafanikio ya baadaye ya timu ya taifa.
The post Kelvin John atwaa tuzo ya Mchezaji Bora Denmark first appeared on SpotiLEO.