KLABU ya Simba imeanza rasmi maandalizi ya msimu mpya wa 2025/26 kwa kuondoka nchini jana Jumatano kwenda Ismailia, Misri kwa kambi ya wiki nne ikiwa ni sawa na siku 28 ili kunoa makali ya nyota wa kikosi hicho wakiwamo wapya Alassane Kante na beki Msauzi, Rushine De Rueck.
Simba iliyomaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita nyuma ya Yanga na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ilikopoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa mabao 3-1 imeondoka kwa mafungu, huku kocha wa kikosi hicho, Fadlu Davids na benchi la ufundi wakichora mchoro mzima.
Katika msafara wa awali ulioondoka jana, wamo baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza akiwamo mfungaji bora wa msimu uliopita, Charles Jean Ahoua aliyepachika mabao 16, Joshua Mutale, Chamou Karabou, Steven Mukwala, Ladack Chasambi, Awesu Awesu, Hussein Abel na Leonel Ateba, huku nyoya mpya akiwa ni Rushine.
Kundi jingine la msafara wa timu hiyo umepangwa kuondoka leo, likihusisha nyota wapya akiwamo Jonathan Sowah na Alassane Kante, ilihali kundi la mwisho litamalizia kesho Ijumaa mara tu baada ya taratibu za mwisho za upatikanaji wa visa kukamilika.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema maandalizi ya safari hiyo yameenda kwa mpangilio mzuri na kambi hiyo inatarajiwa kuwa ya mafanikio makubwa.
“Tumeondoka leo (jana) na kundi la kwanza la wachezaji pamoja na benchi zima la ufundi. Kesho (leo) Alhamisi na keshokutwa (kesho) Ijumaa, wachezaji wengine wakiwamo wapya ambao bado walikuwa wakisubiri taratibu za visa wataondoka kuungana na wenzao,” alisema Ahmed na kuongeza;
“Tumekuwa na wiki moja ya maandalizi hapa Dar es Salaam, lakini sasa tunaingia kwenye sehemu ya pili muhimu zaidi. Tutakuwa Misri kwa wiki nne, kabla ya kurejea mwishoni mwa Agosti kwa ajili ya Simba Day, ambako tutajikita tena kwenye maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza kwa msimu.”
MSIKIE FADLU
Kocha wa Simba, Fadlu Davids, ameweka wazi kuwa kambi hiyo ni mwanzo wa mabadiliko makubwa ndani ya kikosi chake kuelekea msimu mpya na kwamba atatumia siku hizo 28 kukiwapika vyema wachezaji kimbinu kabla ya kuja kuanza kati kwa msimu ujao wa mashindano.
Kocha huyo ambaye amekuwa kwenye mchakato wa ujenzi wa kikosi tangu msimu uliopita ambao Simba ilishika nafasi ya pili kwenye ligi na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika alisema amesoma makosa na sasa wanakwenda kuyarekebisha kwa vitendo.
“Tuna muda wa wiki nne. Hii nafasi ya kuunganisha wachezaji wapya na wale waliopo, kuwajenga kisaikolojia, kimbinu na kimwili,” alisema Fadlu na kuongeza; “Tutafanya mazoezi ya ndani kwa ndani lakini pia tutacheza mechi za kirafiki na timu zenye ushindani ili kuona wapi tumefika. Lengo ni kuwa tayari kwa changamoto yoyote itakayokuja msimu ujao.”
Fadlu aliongeza kuwa kambi hiyo pia ni muhimu kwa kufanyia kazi mbinu mpya ambazo anatarajia kuzitumia kwa ajili ya msimu ujao lakini pia alifichua kufurahia usajili waliofanya.
KAMBI YA MISRI
Simba imekuwa na desturi ya kufanya maandalizi ya nje ya nchi kwa miaka ya hivi karibuni. Kambi za Misri zimewahi kuzaa mafanikio miaka ya nyuma, na msimu ujao klabu hiyo inarejea kwa lengo la kurejesha heshima yake baada ya kutoka patupu msimu uliopita.
Taarifa zinaeleza kuwa Simba imeandaa ratiba kali ya mazoezi ya viwango vitatu: mazoezi ya asubuhi ya kuimarisha stamina, mazoezi ya jioni ya kiufundi, na mafunzo ya kimbinu ya kiakili kwa wachezaji wote.
Pia, mechi nne hadi tano za kirafiki zinatarajiwa kuchezwa dhidi ya timu kutoka Ligi Kuu ya Misri na nyingine kutoka Tunisia ambazo zitakuwa kambini humo wakati huo. Mechi hizo ni sehemu ya tathmini ya benchi la ufundi katika kupima mwelekeo wa wachezaji wapya.
Hadi sasa Simba imemtambulisha nyota mpya mkubwa beki kutoka Afrika Kusini, Rushine, akiwamo kiungo Kante kutoka Senegal, Mohammed Bajaber, Yakoub Suleiman, Rodrigue Kossi, Jonathan Sowah ana Khadim Diaw.
The post HATARIIIII….MASTAA WAPYA WAPEWA SIKU 28 SIMBA….NENO LA FADLU HILI HAPA… appeared first on Soka La Bongo.