Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Profesa Peter Msofe ameonekana kuridhishwa na utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika utekelezaji wa majukumu ya Mazingira hasa usimamizi wa utekelezaji wa Sheria ya Mazingira Nchini.
Hayo yamedhihirika wakati alipotembelea Ofisi za Baraza jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza toka kuteuliwa kwake katika nafasi hiyo ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Mazingira.
Amesema “NEMC pamoja na changomoto zote, bado mmepiga hatua katika suala Zima la usimamizi wa utekelezaji wa Sheria ya Mazingira nchini.
Amesema “NEMC mnafanya kazi, watu wanaona na mnaonekana, licha ya changamoto mnazokumbana nazo, lakini endeleeni kufanya kazi kwa ajili ya manufaa ya Taifa la Tanzania, huku mkilinda Afya zenu dhidi ya Mazingira hatarishi katika Utekelezaji wa majukumu yenu” amesema Prof.Msofe.
Aidha ameainisha mambo matano ambayo watumishi wa NEMC wanatakiwa kuyazingatia katika utekelezaji wa majukumu ambayo ni kuweka uwiano kati ya vihatarishi binafsi na vihatarishi vya Mazingira ya kazi ili kuepuka madhara ya kiafya katika Utekelezaji wa majukumu, kujifunza na kushirikishana ujuzi wa utendaji kazi, ushirikiano mkubwa katika kazi na uvumbuzi katika maswala ya Mazingira ili kuweza kufanya kazi kwa kuendana na ulimwengu wa sasa.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipozungumza ameesema bado NEMC inakabiliana na changamoto katika kutekeleza majukumu yake kutokana na kukosekana kwa Sheria inayotoa Mamlaka kamili ya Utekelezaji ambapo bado mchakato wa kuifanya NEMC kuwa Mamlaka unaendelea.