*Utekelezaji wa mradi wafikia asilimia 98
*Bodi ya nishati Vijijini yasisitiza mradi ukamilike kwa wakati
*Mradi kupunguza matumizi ya nishati isiyo rafiki na mazingira
Njombe
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imetoa kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kwenye mradi wa kuzalisha umeme wa maji Lupali wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 317 unaotekelezwa na shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 1, 2025 na Mjumbe wa Bodi, Bw. James Mabula wakati akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, walipotembelea mradi wa Lupali unaotumia nguvu ya maporomoko madogo ya maji ya mto Lupali katika kuzalisha umeme mkoani Njombe.
Amesema kuwa, fedha zilizotolewa na REA zimewezesha ujenzi wa kituo cha uzalishaji wa umeme na miundombinu ya usambazaji kwenye kituo cha Imiliwaha Sisters Convent pamoja na vijiji vya jirani vya Boimanda, Kitulila na Matola sambamba na kuwezesha tafiti za mradi huo.
“Hii ni pamoja na gharama za utafiti wa awali wa mradi, ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme (11kV) kilomita 23.48 na njia ndogo za kusambazia umeme kwa watumiaji kilomita 30.61,” Amesema Bw. Mabula.
Aidha, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 98 ambapo kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa kizuizi cha maji na mtaro wa kupitisha maji ya mafuriko ambao tayari umekamilika.
Ameongeza kuwa, wamekamilisha ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme (Powerhouse, mfereji wa kurudisha maji mtoni pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha maji na ununuzi wa vifaa vya umeme uliofikia asilimia 90.
Kwa upande wake, Mshauri wa Biashara wa mradi huo, Bw. Malimi Sitta amesema kuwa, mara baada ya mradi kukamilika, umeme utakaozalishwa utauzwa moja kwa moja kwa TANESCO ambapo tayari mkataba wa kuuziana umeme umeshasainiwa.
Ameongeza faida za mradi utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi kwa matumizi ya nyumbani na biashara na kupinguza matumizi ya nishati isiyo rafiki na mazingira.
Ziara hiyo ya REB mkoani Njombe imelenga kupitia utekelezaji wa miradi ya REA inayotekelezwa katika huo sambamba na kupitia changamoto za waendelezaji wadogo wa miradi ya kuzalisha umeme hapa nchini na kupatiwa ufumbuzi.