Na Sophia Kingimali.
Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA) kwa kushirikiana na taasisi ya Policy data Institute wametoa mafunzo kwa wanahabari nchini ya kujilinda dhidi ya mitandao lakini pia kutumia mitandao hiyo kuripoti taarifa sahihi hasa katika kupindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza katika mafunzo hayo Jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema kuwa mafunzo haya ni muhimu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi kwani matukio mengi yanaweza kutokea katika mitandao ikiwemo taarifa zisizo na ukweli ambazo zinaweza kuzua taharuki.
“Mafunzo hayo yanalenga kuwahamasisha waandishi wa habari kujua mbinu bora za kujilinda mtandaoni na kuandaa maudhui ya habari ambayo hayatashusha maadili au kuleta taharuki katika jamii”,Amesema.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, ambapo usalama wa waandishi wa habari unapaswa kuwa kipaumbele.
“Usalama wa waandishi wa habari ni sehemu muhimu ya kuhakikisha kwamba mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa ufanisi na kwa uadilifu. Waandishi wa habari wanapokuwa salama mtandaoni, wanapata nafasi nzuri ya kufanya kazi zao kwa weledi na kwa uhuru.”
Aidha Dkt. Rose ameongeza kuwa, mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi endelevu za TAMWA katika kuhakikisha kwamba waandishi wa habari, hususan wanawake, wanapata maarifa ya kujilinda dhidi ya vitisho vya mtandaoni ikiwemo udanganyifu, kubughudhi na mashambulizi ya mtandaoni.
Pia, amewasisitiza waandishi wa habari kutumia vyombo vya habari na majukwaa ya mtandaoni kwa busara ili kuepuka kueneza habari za uongo au zinazoweza kuchochea machafuko.
“Hatuwezi kupuuza athari za habari potofu. Waandishi wa habari wanayo jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba wanapofikisha habari kwa jamii, wanazingatia ukweli na usahihi,” alisisitiza Dkt. Rose.
Mafunzo hayo yamejumuisha masuala mbalimbali ya usalama mtandaoni, ikiwa ni pamoja na mbinu za kujilinda dhidi ya mashambulizi ya mtandaoni, matumizi salama ya mitandao ya kijamii, na jinsi ya kutambua taarifa sahihi na feki zinazorushwa mitandaoni kutoka kwa vyanzo tofauti.
Wanahabari walioshiriki katika mafunzo hayo wamesema kuwa yamewajengea uwezo mkubwa na wanajiandaa kutumia maarifa hayo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo haya ya TAMWA yanakuja katika kipindi muhimu cha kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, ambapo waandishi wa habari wanatarajiwa kuandika, kuripoti matukio mbalimbali ya kampeni mpaka uchaguzi kwa weledi na kwa uangalifu mkubwa.