Kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Márcio Máximo ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa klabu ya KMC ya Dar es Salaam, amesema Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024 ni fursa muhimu kwa Tanzania kuonesha maendeleo yake katika soka, si tu kwa Afrika Mashariki, bali kwa bara zima la Afrika.
“Nadhani hii ni fursa ya kipekee kwa Tanzania, kwani ardhi ya nyumbani inawakilisha nafasi ya kipekee kwa nchi hii katika mpira wa miguu. Leo hii Tanzania ni moja ya sehemu bora zaidi ya soka katika Afrika hasa ukanda wa Kaskazini na Mashariki kwa sababu ushindani umeongezeka sana,” amesema Máximo.
Akizungumzia mechi ya ufunguzi ikiwakutanisha Taifa Stars dhidi ya Burkina Faso itakayochezwa kesho Agosti 2, 2025, ameeleza kuwa mashindano haya ni jukwaa la kimataifa ambalo linaweza kuwapa wachezaji nafasi ya kujionesha, sio tu kwa makocha na mashabiki, bali pia kwa wadau wa soka kutoka mataifa mbalimbali.
“Kwa wachezaji, hii ni fursa ya kipekee kuonesha uwezo wao mbele ya mashabiki, hasa kwa kuwa mara ya kwanza mashindano haya yanafanyika nyumbani. Natumaini mashabiki watajitokeza kwa wingi kama ilivyokuwa zamani. Hii ni nafasi nzuri kwao kuwa karibu na timu yao ya Taifa.”
Ikumbukwe Máximo akiwa kocha wa timu yetu ya taifa, alishiriki mashindano haya yalipoanza mwaka 2009.