Afisa Habari wa klabu ya Yanga SC, Ali Kamwe, ameibuka na kauli kali kufuatia hatua ya klabu ya Simba SC kutumia picha ya Rais wa Yanga, Hersi Said, katika video yao ya utambulisho wa mchezaji mpya.
Video hiyo, iliyochapishwa na Simba SC kupitia ukurasa wao wa Instagram tarehe 1 Agosti, inaonyesha picha ya Hersi Said ikichanwa, hatua inayoashiria kwamba mchezaji mpya wa Simba aliikataa ofa ya Yanga.
Kitendo hicho kimeibua hasira kali kutoka kwa Yanga SC. Kupitia taarifa rasmi, Ali Kamwe amesema kuwa wamechukizwa sana na matumizi hayo ya picha ya kiongozi wao katika muktadha ambao si wa heshima.
Ameeleza kuwa klabu yao imeshtushwa na kushangazwa na hatua ya Simba kutumia mbinu hizo za kichokozi.
Ali Kamwe amesema kuwa leo atashirikiana na timu ya kidigitali ya Yanga SC kuandaa tangazo maalum lenye lengo la kuwajibu vikali watani wao wa jadi.
Ameeleza kuwa Yanga SC ipo tayari kulipa kisasi kwa staili ya kipekee, na kwamba usiku wa leo mashabiki wa soka watashuhudia utambulisho wa mchezaji mkubwa ambaye ataumiza mioyo ya mashabiki wa Simba SC.
Kwa mujibu wa Kamwe, Yanga SC ina staa mkubwa aliye tayari kutambulishwa rasmi, na hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa klabu hiyo kuonyesha uwezo wake na kuwajibu wale wanaowachokoza.
Mashabiki wa soka nchini sasa wanasubiri kwa hamu kuona hatua hiyo ya Yanga SC, huku ushindani wa jadi kati ya klabu hizi mbili kubwa ukiendelea kuchukua sura mpya mitandaoni.