LICHA ya kuwa kipa bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25 kwa takwimu na hata ushindani wa kimataifa, Moussa Camara alijikuta kwenye sintofahamu kuhusu hatma yake ndani ya Simba.
Tishio la kupigwa chini lilikuwa wazi, si kwa sababu ya kuruhusu mabao 13 kwenye ligi, bali kwa sababu ya mfululizo wa makosa katika mechi muhimu yaliyowagharimu wekundu wa Msimbazi.
Camara, raia wa Guinea, aliweka rekodi ya kuvutia msimu uliopita kwa kutoruhusu bao ‘clean sheets’ katika mechi 19 ligi kuu. Hilo pekee linamtambulisha kama mmoja wa makipa bora waliowahi kupita Ligi Kuu Bara katika miaka ya karibuni.
Lakini, takwimu hizo hazikutosha kuwahakikishia baadhi ya viongozi na mashabiki kuwa bado anastahili kuendelea kubeba mikoba ya kuwa kipa namba moja Simba kwa msimu wa 2025/26.
MAKOSA KWA CAMARA
Achana na kosa la dabi ambalo aliutemea mpira ndani ambao ulikuwa ukionakana kutoka na Yanga ikapata bao pekee la ushindi katika mechi ya kwanza ya dabi, Oktoba 4, 2024, Simba ikiwa nyumbani iliikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa KMC.
Mechi hiyo ilianza kwa matumaini makubwa kwa wekundu hao wa Msimbazi waliokuwa mbele kwa mabao 2-0, lakini ikaisha kwa sare ya 2-2. Mabao yote mawili ya Coastal yalitokana na makosa ya Camara, hali iliyowapa Coastal nafasi za kurudi mchezoni.
NGOMA ALIVYOMNYOOSHEA KIDOLE
Katika mechi ya marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Camara alijikuta kwenye mvutano ndani ya uwanja.
Wakati timu ikihitaji kujilinda huku ikihitaji mabao ya kusawazisha, Camara alifanya uamuzi utata ambao ungeweza kuiangusha Simba kwa mara nyingine. Kosa lake lilimfanya kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma kumjia juu kwa ukali muda mfupi baada ya tukio hilo.
FOFANA KATIKA HESABU
Katika harakati za kuangalia mbadala wa Camara, jina la Issa Fofana kutoka Al Hilal ya Sudan lilianza kutajwa kwa uzito. Fofana ni kipa aliyeonyesha kiwango kikubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, huku pia akiwa na uzoefu mkubwa wa mechi za presha.