Kamishna wa THBUB, Mhe. Nyanda Shuli akizungumza na ugeni kutoka MNCC ulioongozwa na Kamishna Lyka Mtambo Milanzi wa MNCC (waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa tume mbili hizo.
Mhe. Nyanda Shuli wa THBUB na Mhe. kamishna Lyka Mtambo Milanzi wa MNCC (waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe walioambatana nao
………..
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUH) imekutana na kufanya mazungmzo na Tume ya Taifa ya Watoto kutoka Malawi, (Malawi National Children’s Commission – MNCC) ambayo ilifanya ziara yake nchini Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya tume mbili hizo.
Mkutano huo uliofanyika ofisi za THBUB zilizopo Dar es Salaam chini ya uenyeji wa Mhe. Kamishna Nyanda J. Shuli na ujumbe walioongozana nao tume hizo.
Katika mazungumzo yao tume mbili hizo yalilenga zaidi kukuza ushirikiano na kuendeleza uhusiano baina yao hasa katika eneo la kilinda na kutetea haki za watoto.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Kamishna wa THBUB, Nyanda Shuli aliueleza ujumbe wa MNCC kwamba THBUB inashughulikia masuala mbalimbali yanayohusu haki zikiwemo haki za watoto.
Aidha, Kamishna Shuli aliendelea kuuelezea ugeni huo namna ya THBUB inavyofanya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa haki za watoto pamoja na kuwafuatilia watoto walioko gerezani na shule za maadili.
Pia, Kamishna Shuli aliuelezea ugeni huo kuhusu THBUB inavyoanzisha klabu mbalimbali za haki za binadamu katika shule za msingi, sekondari na vyuo pamoja kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa klabu hizo.
Katika hatua nyengine, Kamishna Shuli alielezea jinsi THBUB inavyoendesha kampeni na maadhimisho mbalimbali ya ulinzi wa haki za watoto ikiwemo siku ya mtoto wa Afrika kwa kutumia midahalo, vyombo vya habari kama radio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii.
Vilevile, Kamishna Shule alieleza namna THBUB inavyofanya utafiti wa masuala mbalimbali ikiwemo mambo yanayohusu uvunyifu wa haki za watoto pamoja na kufanya mapitio ya sera na sheria mbalimbali za zinazowahusu watoto.
Kwa upande wake Kamishna wa Tume ya Taifa ya Watoto ya Malawi (MNCC) Mhe. Lyka Mtambo Milanzi, aliishukuru THBUB kwa ukarimu na mapokezi mazuri waliowaonesha yeye na ujumbe alioambatana nao na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Tume mbili hizo.
Kamishna Lyka pia alieleza lengo la ziara yao hiyo hapa Tanzania ni kujifunza kupitia THBUB namna inavyotekeleza majukumu yake kufuatia Malawi kuanzisha Tume mpya inayoshughulikia masuala ya haki za watoto (MNCC) tangu mwezi Septemba, 2024.
Ujumbe kutoka MNCC uliongozwa na Mhe. Kamishna Lyka Mtambo Milanzi pamoja na maafisa wengine wa Tume hiyo alioongozana nao.