Na Hellen Mtereko,
Mwanza
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) imeeleza umuhimu wa uwekezaji katika ujenzi wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na kuwasogezea wananchi huduma hatua itakayosaidia kuepukana na changamoto ya ununuaji wa nishati hiyo kwenye vidumu.
Hayo yamebainishwa Agosti 03, 2025 na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la mamlaka hiyo katika maonesho ya Wakulima Nane Nane ambayo yanafanyika Nyamh’ongolo Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.
Ameeleza kuwa ujenzi wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini unagharama nafuu na masharti ya utekekezaji wa ujenzi huo yanapunguzwa ukilinganisha na mjini.
Kabla ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani nchi ilikuwa na vituo 279 vya mafuta katika maeneo ya vijijini,lakini hadi sasa vituo vya mafuta vimeongezeka na kufikia 515.
“Ongezeko hilo linatokana na kupunguzwa kwa masharti na gharama za ujenzi za vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini,ujenzi wake ni rahisi ukuilinganishwa na maeneo ya mjini”, amesema Mhina
Amesema kwa upande wa vijijini muwekezaji anatakiwa apeleke mhutsari wa Kijiji unaoonesha umiliki wa eneo pia hawahitaji muwekezaji awe na kibali cha mazingira kutoka NEMC bali wanahitaji barua ambayo imesainiwa na Mkurugenzi wa Halmshauri husika ikionesha kituo kipo Kijijini na endapo ujenzi ukifanyika hautaathiri mazingira.