Na Mwaandishi Wetu Lindi
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wamesema Bajaji zaidi ya 5000 zinatumia nishati safi ya gesi badala ya mafuta ya Petroli au diseli l.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka shirka hilo Ally Mlug ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, Ngongo Mkoani Lindi.
“Kwa sasa zaidi ya Bajaji 5000 na mgari 5000 nchini yanatumia nishati safi ya gesi asilia,” amesema.
Amesema Idadi ya vituo vya kujazia gesi asilia kwenye magari na bajaji (CNG stations) vimefika nane kikiwemo kituo Mama cha jijini Dar es Salaam chenye uwezo wa kujaza gesi asilia kwenye magari 1200 kwa siku.
“Ujenzi wa kituo hicho umekamilika na kinatoa huduma ya kujaza gesi kwenye magari, Bajaji , ambapo kimesaidia hata kupunguza msongamano wa vyombo vya moto ambavyo vinatumika nishati hiyo kwenye vituo vingine,” alisema.
Akizungumzia mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia,Mluge amesema nyumba zaidi ya 1,512 na taasisi 13 Dar es Salaam, Lindi na Mtwara zimeunganishwa na matumizi ya nishati hiyo.
Mkakati huo pia umeunganisha viwanda 57 huku mchakato ukiendelea kuunganisha viwanda vingine zaidi.
Mluge amesema mkakati huo wenye lengo la kuunganisha asilimia 80 ya watanzania kwenye matumizi ya nishati safi ya gesi asilia ifikapo 2034 unaendelea katika mkoa wa Lindi, Mtwara na baadae utatekelezwa kwenye mikoa mingine.
Upande wa Lindi Mluge amesema nyumba 470 zinatarajia kuunganishwa kupitia utekelezaji wa mradi wa pili ambao unatakelezwa katika eneo la mnazi mmoja. Mradi wa kwanza uliunganisha nyumba 209.
Mradi huo utaunganisha gesi asilia kwa nyumba 570 eneo la Kisemvule Wilaya ya Mkuranga, Mkoani Mpwani.
Kwa upande wa Mtwara nyumba 420 zimekwisha kuunganishwa na nishati hiyo.
Ili kuhakikisha kuwa Mikakati wa nishati Safi ya kupikia unatakelezwa, TPDC wanashirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini ili kutekeleza malengo ya mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia ifikapo 2034.
Mpango wa shirika (TPDC) ni kuendelea kusambaza nishati hiyo maeneo mengi,” alisema na kuongeza kuwa kwa Sasa TPDC wanashirikiana na Wakala wa vijijini kutekeleza Mikakati.
Mkuu wa wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva amelipongeza shirika hilo kwa kutekeleza kwa vitendo azimio la serikali kusambaza Nishati Safi ya Kupikia kwa mkoa wa Lindi ambapo idadi kubwa ya nyumba zinatumia nishati hiyo ya gesi asilia na kupunguza athari ya uchafuzi wa Mazingira.
“Utumishi wa gesi asilia pia umepunguza gharama ambazo wananchi ambao Sasa wanatumia nishati safi walilazimika kutumia kwenye nishati zenye uchafuzi wa Mazingira,” amesema.