MSANII wa muziki na mtangazaji maarufu, Gift Stanford maarufu kama Gigy Money, ametangaza wazi kuwa hana tatizo namba yake ya simu kutolewa kwa mtu yeyote anayehitaji, akisisitiza kuwa wasanii wanapaswa kusaidiana badala ya kuzuiana fursa.
Gigy Money ameeleza kuwa ni jambo la kawaida kwa watu kuulizana namba za mawasiliano hasa kwa nia ya biashara, na kuonya dhidi ya tabia ya baadhi ya wasanii kubaniana namba au kukwamishana katika nafasi muhimu za kazi.
“Kwanzia leo, ukiombwa namba yangu toa tu. Watu wana biashara zao mjini hapa,” amesema Gigy Money kwa msisitizo, akieleza kuwa kila mmoja ana riziki yake na hapaswi kuizuiliwa kwa sababu ya kutoaminiana au ushindani usio na tija.
Msanii huyo ameweka wazi kuwa anathamini mitandao ya ushirikiano na fursa zinazotokana na kuaminiana kati ya wasanii, wadau wa burudani, na wafanyabiashara.
Kauli hiyo ya Gigy imeibua mjadala mpya kuhusu uwazi na mshikamano katika tasnia ya burudani, ambapo mara kwa mara wasanii wanalaumiwa kwa kujifungia na kukatisha juhudi za wenzao kufanikisha miradi ya pamoja.
The post Gigy Money atoa ruhusa namba yake kusambazwa first appeared on SpotiLEO.