Moshi. Mbunge wa Vunjo anayemaliza muda wake, Dk. Charles Kimei, ameangushwa katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mpinzani wake wa muda mrefu, Enock Koola, katika mchakato wa kuwania tiketi ya kugombea ubunge jimboni humo. Koola ameibuka na ushindi wa kishindo kwa kupata kura 1,999 huku Kimei akijizolea kura 861 kati ya kura halali 4,054 zilizopigwa. Kura hizo zimefanyika mwishoni mwa wiki katika kata mbalimbali za jimbo hilo lililopo mkoani Kilimanjaro.
Ushindi huo kwa Koola unakuja baada ya kumbwaga Dk. Kimei kwa mara ya pili mfululizo katika kura za maoni, licha ya matokeo ya mwaka 2020 kutopelekea uteuzi wake rasmi. Katika kura za maoni za mwaka huo, Koola alipata kura 187 dhidi ya 178 za Kimei, lakini chama kilimteua Kimei kuwa mgombea wake wa ubunge. Hatua hiyo ilizua mijadala miongoni mwa wanachama, baadhi wakieleza kutoridhishwa na uamuzi wa kupuuzwa kwa kura za msingi.
Kwa sasa, macho ya wanachama na wachambuzi wa siasa yako kwa Kamati Kuu ya CCM, wakisubiri kuona kama safari hii chama hicho kitamheshimu mshindi wa kura za maoni au kitarejea tena mchakato wa mwaka 2020. Jimbo la Vunjo lina rekodi ya kuwa na wabunge wanaobadilika kila baada ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwake mwaka 1995, hali inayofanya mchakato wa sasa kufuatiliwa kwa karibu zaidi kisiasa na kijamii.