Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
RAIA wawili wa Sri Lanka, na watanzania watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi yenye shtaka la kuingiza sampuli za dawa za kulevya zenye uzito wa zaidi ya tani 11.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Davies Eric imewataja Washtakiwa kuwa ni Riziki Shaweji(40), Andrew Nyembe(34), Mariam Ngatila(40), Ramadhan Said(57), Godwin Maffikiri(40), pamoja na raia wawili wa Sri Lanka Jagath Prasanna Madduma Wellalage(40) na Santhush Ruminda Hewage(46).
Mbele ya Hakimu Mkazi, Mwandamizi Franco Kiswaga inadaiwa washtakiwa walitenda kosa hilo Julai 15, 2025, katika Bandari kavu ya Said Salim Bakhresa (SSB-ICD) iliyopo eneo la Sokota, Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam
Imedaiwa kuwa, siku na mahali hapo washtakiwa walikamatwa wakiingiza ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dawa aina ya Mitragyna Speciosa zinazofanana kwa madhara sawa na dawa za kulevya, zenye uzito wa Kilo 11,596.43 ambazo ni sawa na zaidi ya tani 11.
Kwa mujibu wa taarifa dawa hizo zinaweza kuwa na madhara sawa au zaidi ya dawa za kulevya aina ya heroin au cocaine.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za za madawa ambazo kwa kawaida zinasikilizwa mahakama Kuu au kwa kupata kibali kutoka kwa DPP.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na washtakiwa wamerudishwa rumande hadi Agosti 19,2025.