Dodoma
Mfuko wa SELF MICROFINANCE FUND (SELF MF), taasisi ya serikali chini ya Wizara ya Fedha, umejipanga kuunga mkono maendeleo ya sekta ya kilimo na kuongeza ajira kwa vijana kupitia huduma rafiki za kifedha, zikiwemo mikopo, elimu ya fedha na bima kwa wakulima na wafugaji.
Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Meneja wa Masoko na Uhamasishaji wa SELF MF, Bi Linda Mshana, alisema taasisi hiyo inalenga kutoa huduma za kifedha zinazowezesha wakulima na vijana kuinua miradi yao ya kiuchumi, hasa katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Tunatoa mikopo yenye masharti rafiki kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili kuwawezesha kukuza shughuli zao. Vilevile, tumeanzisha mpango maalum wa mikopo kwa vijana wasio na ajira ili waweze kuanzisha miradi ya kilimo na kujikwamua kiuchumi,” alieleza Bi Mshana.
Aidha, alibainisha kuwa SELF MF inatoa huduma ya bima kwa wakulima na wasafirishaji wa mazao ili kuwalinda dhidi ya hasara zinazoweza kutokana na uharibifu wa mazao wakati wa usafirishaji. Huduma hizi zimekuwa mkombozi kwa wakulima wengi wanaokabiliwa na changamoto zisizotarajiwa.
“Mbali na mikopo na bima, tunatoa pia elimu ya fedha kwa wananchi ili kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, jambo ambalo linaongeza ustawi wa kiuchumi katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Bi Mshana, dhamira ya SELF MF ni kuhakikisha kila mdau wa kilimo na ufugaji – kuanzia wakulima wadogo hadi vikundi vya vijana – anapata huduma bora na jumuishi za kifedha zitakazosaidia kuongeza tija na kupunguza changamoto zinazowakabili wajasiriamali hususan waliopo vijijini.