Nyota wa Al-Talaba SC ya Iraq, Simon Msuva ameweka wazi matumaini yake kwa Taifa Stars, huku akisisitiza huu ndiyo wakati wa kuvunja rekodi zote mbovu na kutinga fainali ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) ikiwa ni kwa mara ya tatu kushiriki mashindano hayo.
“Ushindi dhidi ya Burkina Faso ni mwanzo mzuri, lakini pia ni ujumbe kuwa wachezaji wetu wamekomaa, wanacheza kwa akili na moyo ya kupambania nchi. Tukiendelea hivi, si ajabu tukaingia fainali,” alisema Msuva
Msuva alisema kuwa wenyeji ni fursa ambayo haitakiwi kupuuzwa kwani mazingira ya nyumbani yanatoa motisha ya ziada kwa wachezaji kufanya makubwa.
“Tupo nyumbani, tuna sapoti ya mashabiki, mazingira tunayajua vizuri. Tunachotakiwa kufanya ni kutumia fursa hii kwa makini. Hatuhitaji miujiza, tunahitaji nidhamu, umoja na mpango wa kweli wa kiufundi. Nafasi ipo, rekodi mpya inawezekana,” alisema.