NIRC: DODOMA
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Bw. Raymond Mndolwa amesema Serikali imefanya maamuzi mahususi kuwekeza katika Kilimo cha Umwagiliaji ili kuweza kuwa na mchango katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mndolwa amesema hayo katika Maonesho ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea viwanja vya Nzuguni Dodoma, wakati wa majadiliano maalumu ya wadau wa kilimo wanaotekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Mjadala huo umeandaliwa na Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), ambapo Mndolwa ametumia fursa hiyo kueleza wajibu wa Tume katika utekelezaji wa Dira na kuchochea ukuaji wa sekta ya Kilimo nchini.
“Tangu kupata Uhuru nchi ilikuwa inategemea mvua katika kilimo na kilimo cha kutegemea mvua uhakika wa kuvuna unakuwa mdogo hivyo Serikali imeamua kuwekeza katika Umwagiliaji na ukiangalia malengo ya Dira yetu katika sekta ya Umwagiliaji unaona namna ukuaji wa sekta ya kilimo utakavyofikiwa kwa kuwa na kilimo cha uhakika, kisichotegemea mvua na hatimaye wananchi kukuza uchumi wao mmojamoja na nchi kufikia uchumi wa kati”, amesema
Ameongeza kuwa mipango ya Tume ni Taifa kuendelea kustahimili mabadiliko ya Tabia ya Nchi pamoja na kujenga hali nzuri ya maisha ya Watanzania kupitia kilimo.
“ Ili kufikia adhima hiyo Tume inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ile mikubwa ya kimkakati ya mabwawa na uchimbaji wa visima ambapo mitambo iliyopo itawafikia wakulima wote kupitia halmashauri zao,”amesema.
Amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha Tume inakuwa na mchango katika utekelezaji wa Dira hiyo.