Yule bundi bado anaendelea kulia kwenye mkataba wa winga Mkongomani wa Yanga, Jonathan Ikangalombo na wakati wowote anaweza kupewa mkono wa kwaheri.
Iko hivi. Ikangalombo hatma yake ndani ya klabu hiyo bado haisomeki kutokana na hesabu tofauti za mabosi wake na benchi la ufundi la timu hiyo.
Yanga imemuita mezani Ikangalombo wakianza mazungumzo mapya ya kumsitishia mkataba baada ya winga huyo KUGOMA kutolewa kwa mkopo.
“Kwa sasa tunaendelea na majadiliano ya kuachana na Ikangalombo, kuna wakati tuliona kama anaweza kubaki, lakini tulipokubaliana tumpe mkataba Doumbia hapo ni wazi tulijikuta tunatakiwa kuachana naye Ikangalombo, maana tunakuwa tumezidisha wachezaji wa kigeni.
“Kuna watu tunawatafuta na kama kocha akiwapata awe mmoja basi tutalazimika kumtoa kwenye mfumo Yao ambaye ni wasiwasi kama atacheza nusu ya msimu wa kwanza, bado hajapona sawasawa.”
Mbali na kuzidisha idadi ya wachezaji wa kigeni, Yanga inapiga hesabu za kuongeza kiungo mmoja mkabaji au beki wa kati.