DAR ES SALAAM: Baada ya kuachia rasmi wimbo wake mpya ‘Amanda’, msanii wa Bongo Fleva Zuchu ameibua mjadala mkali mitandaoni huku baadhi ya mashabiki wakionesha kutoridhishwa na mwelekeo mpya wa kimuziki aliouchukua.
Wimbo huo, ambao umetoka katika matoleo mawili (clean na explicit) umetayarishwa na S2kizzy na kuwasilisha ladha tofauti kabisa na ile ambayo mashabiki wamezoea kutoka kwake.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Zuchu hakuacha jambo hilo kupita kimya. Ametoa tamko kali kwa wanaomkosoa mabadiliko yake ya kisanii, akisisitiza kuwa hayuko tayari kurudi nyuma kwa ajili ya mashabiki wasiokubali safari yake ya ubunifu mpya.
“This is the new me. I will be as versatile as I want to be. Na kama unahisi mabadiliko haya hayakufai, nakushauri uniache tu sasa,” ameandika Zuchu kwa ukakamavu.
Baadhi ya mashabiki wamepinga mwelekeo wa Amanda, wakidai kuwa ni tofauti mno na Bongo Fleva ya kawaida. Lakini kwa upande wake, Zuchu anaona huu ni wakati wa kuvunja mipaka ya mazoea na kuchunguza upeo mpya wa sanaa.
“Nimechoka kuimba vitu vile vile kila siku… Kama unapenda msanii kwa vigezo vya Grammy, feel free kushabikia mwingine,” ameongeza.
Akiwashukuru mashabiki wanaomuunga mkono kwenye safari hii mpya, Zuchu ametoa ujumbe wa upendo na matumaini:
“I love you. Funga mkanda, maana safari ndo kwanza imeanza.”
Je, wimbo wa “Amanda” ni hatua ya ubunifu wa kimataifa au umetoka nje ya mwelekeo wa Bongo Fleva?
Unamshauri nini Zuchu kwenye safari yake hii mpya ya kisanii?
The post Zuchu awatolea uvivu wanaomkosoa first appeared on SpotiLEO.