

Dar es Salaam, 4 Agosti 2025 – Benki ya Stanbic Tanzania imemaliza rasmi Kampeni yake ya Salary Switch kwa kufanya droo ya tatu na ya mwisho katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam. Tukio hili limeashiria hatua muhimu katika safari ya benki kusherehekea uaminifu wa wateja wake na kuwazawadia wale walioungana nayo.
Katika droo hiyo ya mwisho, wateja 30 walishinda zawadi za pesa taslimu, ambapo tukio hilo lilishuhudiwa na Judith Wililo, mwakilishi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, pamoja na waandishi wa habari kuhakikisha uwazi na uaminifu katika mchakato mzima.
Kampeni ya Salary Switch ilianzishwa kwa lengo la kuwahamasisha wafanyakazi walio kwenye ajira rasmi kuhamisha mishahara yao kuingia kupitia akaunti za Stanbic. Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, jumla ya washindi 90 wamepokea zawadi za hadi TZS 500,000 kila mmoja kupitia droo za kila mwezi.
Akizungumza wakati wa droo ya mwisho, Sarah Odunga, Meneja wa Thamani kwa Wateja Stanbic Bank Tanzania, alisema: “Tunajivunia kufanikisha hitimisho la kampeni ya Salary Switch. Kampeni hii haikuwa tu kuhusu zawadi, bali ilikuwa ni fursa ya kuimarisha uhusiano wetu na wateja na kuonyesha thamani halisi ya huduma za kibenki tunazotoa.”
Aliongeza kwa kusisitiza faida zaidi walizonufaika nazo wateja walioungana na kampeni hiyo. “Wateja waliopitisha mishahara yao kupitia Stanbic walifunguliwa milango ya huduma za kifedha zinazowahusu binafsi, urahisi wa kufanya miamala kidigitali, pamoja na usaidizi wa kifedha unaowawezesha kufikia malengo yao ya kifedha – iwe ni kuwekeza kwenye ndoto zao au kukidhi mahitaji ya kila siku.”
Katika kumalizia hotuba yake, alihamasisha Watanzania kujiunga na huduma za Stanbic. “Tunawaalika Watanzania wote kujiunga nasi na kujionea tofauti. Tukiadhimisha miaka 30 ya kukua pamoja na Watanzania, dhamira yetu inaendelea kuwa ni kutoa huduma za kifedha jumuishi, zinazohusiana na maisha ya watu, na zenye kuwainua kiuchumi.”
Kampeni ya Salary Switch ni moja ya mikakati mingi ya Stanbic Bank inayolenga kuleta ushirikishwaji wa kifedha na kutoa thamani ya muda mrefu kwa wateja wake nchini Tanzania.