Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha National League for Democracy (NLD) kimezindua rasmi Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu 2025, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyowasilishwa Agosti 6 na uongozi wa chama hicho, Ilani hiyo inatajwa kama dira na mwelekeo wa kisera kwa mgombea urais kupitia tiketi ya NLD, Doyo Hassan Doyo, kwa ajili ya kuomba ridhaa ya kuwaongoza Watanzania katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Ilani ya NLD imejengwa juu ya misingi ya Uzalendo, Haki na Maendeleo, na imejikita katika vipaumbele vinne vikuu vinavyolenga kuleta mabadiliko ya kweli na maendeleo jumuishi kwa kila Mtanzania” imesema taarifa hiyo iliyotolewa na idara ya Itikadi, Uenezi na Mahusiano ya Umma ya Chama hicho.
Kimsingi Ilani hiyo imejielekeza katika vipaumbele vikuu vinne ambavyo ni ajira kwa wote, Elimu Bora na Jumuishi, Afya kwa Maendeleo ya Taifa, pamoja na Miundombinu ya kukuza uchumi.
Kuhusu vipaumbele vilivyopo katika Ilani hiyo ni ajira kwa wote ambapo NLD inatambua changamoto ya ukosefu wa ajira, hususan miongoni mwa vijana. Kupitia ilani hiyo chama kinapendekeza mikakati ya kuanzisha viwanda vidogo na vya kati, kuimarisha sekta ya kilimo cha kisasa, pamoja na kuwezesha vijana na wanawake kupitia mikopo, mafunzo, na ujasiriamali.
Lengo. Kupunguza utegemezi, kuongeza uzalishaji wa kitaifa, na kukuza uchumi wa wananchi mmoja mmoja.
Pia Ilani hiyo imeweka kipaumbele cha elimu bora na jumuishi kwani NLD inaamini kuwa elimu ni nguzo ya ustawi wa taifa. Ilani ya chama inalenga kuhakikisha elimu bora, inayopatikana kwa wote bila ubaguzi wa kiuchumi au kijamii, huku mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji yakiimarishwa, pamoja na maslahi ya walimu kupewa kipaumbele.
Lengo. Kujenga kizazi chenye maarifa, ujuzi na maadili kwa ajili ya mustakabali wa taifa.
Aidha kipaumbele kingine ni afya kwa maendeleo ya Taifa ambapo Ilani ya NLD inalenga kuimarisha huduma za afya kwa kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, miundombinu ya afya, pamoja na kupanua wigo wa bima ya afya kwa wananchi wote wakiwemo wa kipato cha chini.
Lengo. Kujenga jamii yenye afya njema, yenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Pia Miundombinu ya Kukuza Uchumi kwa kuwa NLD imejipanga kuwekeza katika barabara, reli, nishati, na teknolojia ya mawasiliano kwa lengo la kuunganisha Watanzania, kupunguza gharama za uzalishaji, na kuongeza ushindani wa taifa katika soko la kikanda na kimataifa.
Kupitia Ilani hii, Chama cha NLD kinaweka mbele matumaini ya Watanzania kwa kutangaza ajenda ya mabadiliko ya kweli, yanayolenga watu, uchumi, na ustawi wa taifa.
Kwa msingi huo, NLD kinawaomba Watanzania wote kuungana na kuunga mkono mwelekeo mpya wa Taifa, kwa kumpa Mhe. Doyo Hassan Doyo ridhaa ya kuwaongoza katika kulijenga taifa lenye Uzalendo, Haki, na Maendeleo kama sehemu ya kuleta usawa na fursa kwa Watanzania wote.