DAR ES SALAAM: TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajia kushuka dimbani leo kusaka ushindi wa pili katika mchezo dhidi ya Mauritania kundi B, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mchezo huo utachezwa saa 2:00 usiku wa saa za Afrika Mashariki. Tayari Tanzania ilishinda mchezo wa kwanza wa ufunguzi dhidi ya Burkina Faso wa mabao 2-0 katika michuano hiyo ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN).
Lakini kabla ya mchezo huo, mapema saa 11:00 jioni Burkifaso itacheza na Central Afrika kwenye Uwanja huo wa Mkapa.
Tanzania ndiye kinara wa kundi kwa pointi tatu ikifuatiwa na Mauritania pointi moja ilizovuna katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Madagascar baada ya sare ya bao 1-1 huku Central Africa na Burkinfaso zikiwa hazina pointi.
Mara ya mwisho Stars na Mauritania zilikutana mwaka 2017 katika michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) nchini Afrika Kusini na kutoka sare ya bao 1-1.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars Hemedi Morocco , amesema kila mchezo kwao ni kama fainali wamejipanga vizuri kuhakikisha wanashinda.
“Naamini sana katika kupata ushindi haijalishi tutafunga magoli mangapi cha msingi ni kupata ushindi,” amesema Morocco.
Stars inahitaji kushinda kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya robo fainali.
The post Stars kusaka ushindi wa pili leo first appeared on SpotiLEO.