Meneja wa TIRA kanda ya kaskazini, Bw. Bahati Ogolla akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya nanenane katika viwanja vya Themi Njiro.
……………
Happy Lazaro, Arusha
Arusha. Wananchi wametakiwa kutembelea banda la Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya nanenane Njiro kwa ajili ya kupata elimu juu ya huduma mbalimbali za bima zinazotolewa na mamlaka hiyo.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Meneja wa TIRA kanda ya kaskazini, Bw. Bahati Ogolla wakati akizungumza kwenye maonesho ya nanenane katika viwanja vya Themi Njiro .
Amesema kuwa, Mamlaka hiyo imeshiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kuelimisha wananchi kuhusu huduma wanazotoa ikiwemo usajili wa watoa huduma za bima. Aidha, ametoa rai kwa wananchi kutembelea ‘mtaa wa bima” kwenye maonesho hayo ili wakutane na watoa huduma za bima kwa ajili ya kujipatia kinga ya bima dhidi ya majanga mbalimbali ikiwemo bima za kilimo, uvuvi na mifugo.
Amesema kuwa, bima ni mpango unaotoa fidia endapo janga litatokea kwa mkatabima ambapo fidia hiyo hutolewa na kampuni ya bima.
Ameongeza kuwa, bima imegawanyika katika makundi mawili ambapo kuna bima ya muda mrefu au bima ya maisha,ambazo muda wake ni zaidi ya mwaka mmoja na bima ya muda au bima ya kawaida ambayo muda wa uhai wa mkataba hauzidi mwama mmoja mfano ,bima za magari, moto, meli, ndege, wizi, dhima na ajali.
Bw. Ogolla amewataka wakulima kuchangamkia fursa ya kukata bima ya kilimo kwani endapo mazao yao yatapatwa na ukame ama mafuriko yakaharibu mazao kampuni ya bima inalipa fidia.
“Nawaomba sana wananchi wafike kwenye banda letu hapa kwa ajili ya kupata elimu kuhusu maswala ya bima kwani bima ina manufaa makubwa sana kwenye shughuli za wananchi kwani ikitokea janga bima ipo kuwafidia.”amesema Bw.Ogolla.
Ameongeza kwamba “Ukiwa na bima ni fursa kubwa kwani ni ajira pia na unaweza kuwa wakala wa bimana inatoa ajira ya kujiajiri na hata kuajiri wengine .”amesema