
Mkurugenzi wa Bodi ya maji Bonde la Pangani ,Injinia Segule Segule wakati akizungumza kwenye banda lao katika.maonesho ya nanenane Njiro
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Wananchi wametakiwa kuwa mabalozi wazuri wa kudhibiti uchimbaji holela wa visima vya maji unaofanyika bila kuwa na kibali kutoka bodi ya maji bonde la Pangani jambo ambalo linaweza kuleta athari kubwa kwa jamii.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi wa Bodi ya maji Bonde la Pangani ,Injinia Segule Segule wakati akizungumza kwenye banda lao katika.maonesho ya nanenane yanayoendelea katika viwanja vya nanenane Njiro .
Injinia Segule amesema kuwa, wananchi wanapaswa kufahamu kuwa ,ni kosa kisheria kuchepusha maji kutoka katika chanzo chochote cha maji,kuchimba visima virefu au kutiririsha maji taka katika vyanzo vya maji bila kuwa na kibali kutoka bodi ya maji .
Ameongeza kuwa, mtu yoyote mwenye uhitaji wa kutaka kuchimba kisima anatakiwa kufika katika ofisi hizo kwa ajili ya kupewa utaratibu ndo maana wapo katika maonesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kufahamu sheria na taratibu mbalimbali .
“Hatutaki kabisa kuona visima vinachimbwa kiholela kwani huko ni kukiuka sheria na taratibu zilizowekwa na kila mwananchi akiona mtu yoyote anachimba kisima ana haki na wajibu wa kuhoji amepata wapi kibali.cha kuchimba na kama hana tunawaomba wafike kwenye ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kwani jukumu la kufuatilia ni la kwetu sote ,hivyo kwa pamoja naomba tushirikiane kufanya hivyo.”amesema .
Amesema kuwa, endapo kutakuwa na ujenzi holela wa kuchimba visima hivyo bila kufuata sheria zilizopo zinaharibu ubora wa maji chini ya ardhi ,unaweza kupata magonjwa ya matumbo pia,wakati mwingine mimba zinatoka hovyo na hiyo ni kutokana na kutumia maji ambayo hayajapimwa ubora wake hivyo ili kuepukana na hayo yote kila mmoja anatakiwa kuwa mlinzi .
Segule ameongeza kuwa, wameweza kufikia idadi kubwa sana ya watu katika kutoa elimu juu ya uchimbaji holela na kwa Tanzania nzima wameweza kufikia watu zaidi ya milioni na bado maboresho yanaendelea katika kuhakikisha elimu unawafikia watu wengi zaidi ili waweze kufuata sheria .
Amefafanua zaidi kuwa, bado wanaendelea na kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji .
‘Changamoto tuliyonayo kwa sasa ni mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo kwa kiwango kikubwa yanaathiri sana vyanzo vya maji ambapo tunaendelea kujengeana elimu na uelewa zaidi wa kutunza mazingira. “amesema .
“Kila mwananchi anatakiwa kushiriki kwenye ngazi ya jamii na wao wenyewe waweze kuchukuliana hatua endapo wakiona mwananchi yoyote amejenga ndani ya vyanzo vya maji wahakikishe wanatoa taarifa katika mamlaka husika ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.”amesema Injinia Segule .
Amefafanua kuwa watumiaji wa maji wenyewe wana wajibu mkubwa wa kutunza maji ,na wao kuwa walinzi kwa wale wote wanaoingiza mifugo kwenye kingo za maji na kamwe wasichoke kuwa walinzi wa Miundombinu ya maji ili iendelee kubaki salama kila wakati.
Ameongeza kuwa, dira ya Bodi ya maji bonde la Pangani ni kuwa Bonde bora Afrika linalotekeleza usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na kutoa fursa na faida sawia za maji kwa jamii iliyopo kwenye bonde .
Amesema kuwa, dhamira kubwa ni kuzisimamia rasilimali za maji kwa kuziwezesha kutumika kwa ufanisi na kuwa endelevu kwa kuzingatia misingi ya ushirikishwaji kwa wadau na utawala bora
Bonde la Pangani ni moja ya mabonde tisa nchini na ndio bonde la kwanza kuundwa mwaka 1991 chini ya sheria ya matumizi ya maji ya mwaka 1974 ,sheria hii ilifutwa na sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji no.11 ya mwaka 2009 ,pamoja na maboresho yake ya sheria no .8 ya mwaka 2022.