LANCASHIRE: Burnley wamekamilisha usajili wa kiungo wa kati wa Ufaransa Lesley Ugochukwu kutoka Chelsea kwa ada ya zaidi ya Pauni milioni 20 huku Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 akisaini mkataba wa miaka mitano kuvinjari Turf Moor. Ada hiyo ya usajili imetajwa kukaribiana na ada ya Pauni milioni 23.2 ambayo Chelsea walilipa kumsajili Ugochukwu kutoka Rennes mwaka 2023.
“Nilijisikia vizuri mara tu nilipofahamishwa kuhusu nia ya klabu hii kunisajili, nilikuwa na hamu ya kusikia zaidi kuhusu mpango huo. hivyo nilizungumza na meneja na Maxime (Maxime Esteve) wote walikuwa na uhakika mkubwa kuhusu klabu na mwelekeo wake naona ni hatua sahihi kwangu” – Ugochukwu alisema.
Ugochukwu alikuwa ‘kuni ya ziada’ kwenye majiko ya Stamford Bridge huku Chelsea wakijaribu kuuza wachezaji kadhaa wakiwemo Waingereza Raheem Sterling na Ben Chilwell wanaofanya mazoezi kando na kikosi cha kwanza cha Enzo Maresca.
Ugochukwu alikaa Chelsea kwa miaka miwili na kucheza mechi 15 pekee kwenye mashindano yote katika msimu wake wa kwanza kabla ya kujiunga na Southampton kwa mkopo wa msimu mzima wa 2024/25.
Burnley pia wako kwenye mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji wa Chelsea mwenye umri wa miaka 23 Armando Broja. Vyanzo vya habari vinasema kuwa uhamisho huo unaweza kuwa na thamani ya hadi Pauni milioni 20 lakini dau kamili halijathibitishwa.
The post Burnley yang’oa ‘mido’ ya Chelsea first appeared on SpotiLEO.