FRANKFURT, KLABU ya Eintracht Frankfurt imetangaza kumsajili Winger wa Kijapani Ritsu Doan katika harakati za kuimarisha kikosi chao kilichopungukiwa nguvu baada ya kumuuzaji wa Hugo Ekitiké wakati huu ikijiandaa kurudi kwenye Ligi ya Mabingwa.
Doan anajiunga na miamba hiyo ya Bundesliga kwa mkataba wa miaka mitano kutoka klabu nyingine ya Ujerumani Freiburg, ambapo alikuwa mfungaji bora na mabao 10 akiisaidia timu yake kumaliza watano kwenye Bundesliga.
“Nimefurahiya sana kuwa hapa Siwezi kusubiri kucheza mbele ya mashabiki wazuri wa klabu hii nzuri.” Doan alisema katika ujumbe wa video uliotafsiriwa kwa mashabiki wa Frankfurt.
Frankfurt wanarudi kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu baada ya kumaliza wa tatu kwenye Bundesliga lakini watakuwa na sura mpya katika eneo la ushambuliaji baada ya mshambuliaji wao Hugo Ekitiké kuuzwa Liverpool kwa ada ya pauni milioni 69.
Doan mwenye umri wa miaka 27 anatarajiwa kushirikiana na mchezaji mpya mwingine mshambuliaji wa zamani wa Mainz Jonathan Burkardt katika jukumu la ushambuliaji ili kuziba pengo la Ekitiké.
Doan alishinda Kombe la Uholanzi na PSV Eindhoven mwaka 2022 na amecheza michezo 57 kwa timu ya kitaifa ya Japan. Hiyo ni pamoja na michezo yake yote kwenye Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar na kuwa sehemu muhimu ya kampeni ya kufuzu Kombe la Dunia la mwaka ujao Marekani, Canada na Mexico.
Huenda winga huyo akacheza mchezo wa kwanza Frankfurt Agosti 17 katika mchezo wa Kombe la Ujerumani dhidi ya Engers ya ligi Daraja la tano. Mchezo wa kwanza wa Bundesliga wa msimu wa Frankfurt ni siku sita baadaye nyumbani kwa Werder Bremen.
The post Frankfurt yaandaa ‘kosi’ la UEFA first appeared on SpotiLEO.