AALBORG, Denmark, MSHAMBULIAJI Mtanzania, Kelvin John, amefunga goli la ushindi na kuiwezesha timu yake ya Aalborg BK ya Denmark kuondoka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Vendsyssel katika mchezo wa mtoano wa Kombe la LandsPokal.
Mchezo huo ulidumu kwa dakika 120 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Kelvin John ndiye aliyefunga bao la ushindi dakika ya 113, na kuiliza timu pinzani na kuibeba Aalborg kufuzu hatua ya 32 bora ya mashindano hayo.
Video iliyotolewa kutoka uwanjani inaonesha namna mchezaji huyo wa kimataifa akishangilia pamoja na mashabiki waliokuwa wakimshangilia kwa wimbo, kutokana na mchango mkubwa aliotoa kwa timu hiyo.
Kelvin John anaendelea kujizolea sifa kubwa barani Ulaya na ni mmoja wa wachezaji vijana wa Tanzania wanaoonesha uwezo mkubwa na kuleta heshima kwa taifa.
Kwa sasa Aalborg inajiandaa kuendelea na safari ya Kombe la LandsPokal huku wachezaji kama Kelvin John wakitarajiwa kuendelea kuonesha ubora.
The post Kevin John aibeba Aalborg Kombe la Landspokal first appeared on SpotiLEO.