KOCHA Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids amesema kuwa wamefanya maboresho makubwa kwenye kikosi kwa kupata saini za wachezaji ambao watakuwa na kazi kupambana kwenye mashindano ambayo watashiriki.
Simba SC msimu wa 2024/25 ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika na kugotea hatua ya fainali ikiwa nafasi ya pili na bingwa alikuwa RS Berkane. Msimu wa 2025/26 Simba SC itapeperusha bendera kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Fadlu ameweka wazi kuwa watakuwa kwenye aina tofauti ya mashindano ambayo yanahitaji ushindani mkubwa na aina ya wachezaji waliopo watakuwa na kazi kupambania ushindi.
“Unaona kuna wachezaji ambao wamesaini kwenye kikosi. Ni aina ya wachezaji wazuri ni saini nzuri ambazo zipo kwenye kikosi. Tutakuwa kwenye mashindano tofauti msimu huu ukiachana na ligi tutakuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Aina ya ushindani kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni tofauti na kwenye Kombe la Shirikisho Afrika hivyo muhimu ni kuwa imara na tayari kwa ajili ya ushindani kwenye mechi zetu ambazo tutacheza.
“Kambi ambayo ipo kwa sasa ninaona tunaendelea vizuri kuna mechi ambazo tutacheza kwa ajili ya kuwa imara zaidi hivyo bado tuna muda wakufanya maandalizi zaidi.”
Miongoni mwa wachezaji wapya ambao wamesajiliwa Simba SC ni Jonathan Sowah mshambuliaji aliyekuwa Singida Black Stars, Abrahm Morice, beki wa kushoto Anthony Mligo aliyekuwa ndani ya Namungo FC.