ISMAILIA, Misri: KIUNGO wa klabu ya Simba Mzamiru Yasini amesema maandalizi ya kikosi hicho kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu yanakwenda vizuri nchini Misri, ambako wapo kambini kwa wiki moja sasa.
Aidha, amesema wachezaji wote wameanza kuonesha makali yao kiasi kwamba kama wataendelea hivyo hadi kuanza kwa mashindano yajayo watakuwa moto.
Akizungumza kutoka Ismailia, Misri, Mzamiru amesema kila mchezaji anajituma kwa kiwango kikubwa, hali inayoashiria msimu ujao kuwa na mafanikio kama hali hiyo itaendelea.
“Maandalizi yanakwenda vizuri. Kila mtu anajitolea na kuonesha ubora wake kwa mwalimu. Nimefurahishwa na morali ya timu na mshikamano uliopo,” alisema Mzamiru.
Kuhusu wachezaji wapya, Mzamiru amesema wamepokelewa vizuri kambini na wameonesha kujichanganya na kikosi kwa haraka, jambo linaloimarisha zaidi umoja ndani ya timu.
“Tumewapokea wachezaji wapya vizuri na wao pia wamepokea uwenyeji wetu vizuri. Tunaunganisha nguvu pamoja. Naamini msimu ujao utakuwa mzuri sana,” aliongeza.
Simba ipo kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano ya kimataifa, ikijiandaa ratiba ngumu inayohitaji kikosi bora na kilichoiva mapema.
The post Mzamiru: Msimu ujao moto first appeared on SpotiLEO.