Dar es Salaam, Agosti 6, 2025 — Bao la dakika ya 89 lililofungwa na beki mahiri Shomari Kapombe limeipa Taifa Stars ushindi wa pili mfululizo katika Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024), baada ya kuichapa Mauritania kwa bao 1-0 katika dimba la Benjamin Mkapa.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulionekana kuelekea sare tasa kabla ya Kapombe kutokea kama shujaa wa Stars kwa kupachika bao safi dakika za lala salama na kuihakikishia Tanzania pointi tatu muhimu.
Kwa ushindi huo, Stars inaendelea kuongoza Kundi B kwa alama 6 baada ya michezo miwili, ikiwa katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Mashabiki waliofurika uwanja wa Mkapa walishangilia kwa nguvu, huku kocha mkuu wa Taifa Stars, Hemed Morocco, akiwapongeza wachezaji kwa nidhamu na juhudi waliyoionesha hadi dakika ya mwisho.
Mchezo unaofuata wa Stars unatarajiwa kuwa dhidi ya Guinea, ambapo ushindi utaihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali bila kusubiri matokeo ya mechi nyingine.