
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la WHI, Mwabuponde amesema lengo ni kuwahamasisha wananchi kuwa sehemu ya wawekezaji katika sekta ya nyumba kwa njia rahisi, salama na inayowapa faida ya uhakika kwa muda mrefu.
“Tunawahamasisha wananchi waje wafahamu Faida Fund ni nini, inafanya kazi vipi na ni namna gani wanaweza kuwekeza kuanzia kiwango kidogo kabisa. Mfuko huu unamuwezesha Mtanzania wa kawaida kumiliki hisa katika nyumba mbalimbali zinazojengwa na WHI nchi nzima,” amesema Mwabuponde.
Ameongeza kuwa kupitia mfuko huo, mwekezaji anaweza kujipatia kipato cha mara kwa mara kupitia gawio la faida linalotokana na mapato ya upangishaji wa nyumba hizo, bila ya kulazimika kuwa na kiasi kikubwa cha mtaji kama ilivyo katika miradi mikubwa ya maendeleo.
Aidha, Mwabuponde amewakaribisha watu wote wanaotembelea maonyesho hayo ya Nanenane kutembelea banda la Watumishi Housing Investments ili wapate elimu ya kina kuhusu umiliki wa nyumba kwa bei rafiki pamoja na uwekezaji kwenye Faida Fund.
Watumishi Housing Investments ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa lengo la kuwezesha watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kumiliki nyumba kwa gharama nafuu pamoja na kuwekeza katika sekta ya makazi nchini Tanzania.