::::::::::
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) limetoa mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, ikiwa ni juhudi za kuwajengea uelewa kuhusu shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na shirika hilo nchini Tanzania.
Mafunzo hayo, ambayo yalifanyika jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii, yalienda sambamba na ziara ya waandishi hao katika Shule za Mafunzo ya Ufundi Yombo kwa Watoto na Watu Wazima Wenye Ulemavu — mradi unaofadhiliwa na JICA.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yuichi Mikami, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanahabari kupata uelewa wa kina kuhusu shughuli za JICA na Ubalozi wa Japani nchini Tanzania, ili waweze kuueleza umma kwa usahihi.
“Ni muhimu kwa wanahabari kufahamu kazi tunazozifanya ili kusaidia kuhabarisha jamii kwa njia sahihi,” alisema Balozi Mikami.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania, Ara Hitoshi, alisema shirika hilo lina maono ya “Kuongoza Dunia kwa Uwaminifu na Mahusiano ya Watu kwa Watu”.
Alisema kwa zaidi ya miaka 60, JICA imekuwa ikishirikiana na Watanzania katika kubadilishana ujuzi na kuendeleza maendeleo ya pamoja.
Katika semina hiyo, waandishi wa habari waliwasilishwa mada mbalimbali, ikiwamo:
“Ushirikiano wa Kuaminiana na Mafanikio: Kufanya Kazi na Japani na JICA” (Trust, Partnership and Achievements: Working with Japan and JICA)
na
“JICA Tanzania na Shughuli Zake katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mpango wa Wajitolea wa JICA” (JICA Tanzania Office and Its Activities, 60th Anniversary of JICA Volunteer Program).
Aidha, waandishi walitembelea mradi wa shule za ufundi Yombo, unaolenga kuwasaidia watoto na watu wazima wenye ulemavu kupata elimu ya ufundi stadi, ikiwa ni sehemu ya miradi ya msingi ya maendeleo inayofadhiliwa na JICA.
Mwaka huu, JICA inaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Wakujitolea kutoka Japan (JOCV), ambao umechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kijamii na maendeleo baina ya Japan na Tanzania.
Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali wakiendelea kusikiliza ma wasilisho yalitolewa kwenye semina hiyo iliyofanyika Dar es salaam .
PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY