Baadhi ya Wakulima ambao ni Wanachama wa Chama cha Akiba na Mikopo Muungano Gumbiro Saccos kilichopo kijiji cha Mtyangimbole Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma wakichambua mahindi kwa ajili ya kuuza kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA(Picha na Muhidin Amri).

Mwenyekiti wa Muungano Gumbiro Saccos Elia Tenga kushoto,akisimamia zoezi la kuchambua mahindi ya Wakulima kwa ajili ya kuuza kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA)Kanda ya Songea(Picha na Muhidin Amri)
Na Mwandishi Maalum,Madaba
BAADHI ya wakulima wa mahindi katika Kijiji cha Mtyangimbole Halmashauri ya Madaba Wilayani Songea,wameishukuru Serikali kwa kuweka ruzuku katika mbolea hivyo kusaidia kupungua kwa gharama za uzalishaji na kulima kwa tija.
Wamesema, mbolea za ruzuku zimewezesha kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo kutoka Sh.160,000 hadi 70,000 mfumo mmoja wa kilo 25 na kuhamasisha watu wengi wakiwemo vijana kuanza kulima mahindi kibiashara.
Mkulima wa kijiji hicho Wilgis Luambano alisema,punguzo hilo ni ishara nzuri ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuwajali wakulima ambao walishaanza kukata tamaa ya kuendelea na kilimo cha mahindi kutokana na gharama kubwa za uzalishaji hasa mbolea iliyokuwa ikuzwa kwa bei kubwa.
“Kabla ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan kuweka ruzuku kwenye mbolea,wakulima wengi tulipunguza ukubwa wa mashamba yetu na kulima eneo dogo kutokana na kushindwa kumudu gharama za pembejeo hususani mbolea ambazo ziliuzwa kwa bei juu kati ya Sh.120,000 hadi 170,000 huku mazao yakiuzwa bei ya chini”alisema Luambano.
Alieleza kuwa,kutokana na mbolea kuuzwa kwa bei ya juu hata uzalishaji kwenye mashamba yake ulikuwa mdogo kwani katika ekari moja alivuna gunia 10 hadi 15 lakini kutokana na kupata mbolea za ruzuku uzalishaji umeongezeka hadi kufikiwa gunia 25 kwa ekari moja.
Mkulima mwingine Mwanarabu Pili,amemshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuwajali katika shughuli zao za kilimo kwa kutoa pembejeo za ruzuku kila unapofika msimu wa kilimo ambazo zimechochea uzalishaji wa mahindi kwa wakulima wa kijiji hicho.
“Kabla ya mpango wa mbolea wa mbolea za ruzuku sisi wakulima hatukupata mafanikio makubwa katika uzalishaji,baadhi yetu tulishindwa kumudu bei ya mbolea,tunamshukuru sana Rais Samia kwa kutujali sisi wakulima wadogo wa mahindi”alisema Pili.
Meneja wa Chama cha akiba na mikopo Muungano Gumbiro Saccos Theoford Sefu alisema,Chama hicho kinajihusisha na upokeaji wa akiba na kutoa mikopo ya kilimo kwa wanachama na katika kipindi cha miaka minne kimefanikiwa kuzalisha mahindi kwa wingi ikilinganisha kabla Serikali ya awamu ya sita haijaingia madarakani.
Alisema,miaka ya nyuma uzalishaji wa mahindi kwa wakulima haukuwa mkubwa kutokana na pembejeo hasa mbolea kuuzwa kwa bei ya juu, hali iliyopelekea baadhi ya wakulima kushindwa kununua na wengine kuacha kutumia mbolea kwenye mashamba yao jambo lililosababisha kushuka kwa uzalishaji.
Alisema,baada ya Serikali kuweka ruzuku kwenye mbolea uzalishaji umeongezeka kutoka gunia 25 hadi 35 kwa ekari moja na ameipongeza Serikali kwa jitihada kubwa inayofanya kuwekeza kwenye kilimo ambayo ni uti wa mgongo katika Mkoa wa Ruvuma.
“Kwa upande wa soko tunaishukuru Serikali kupitia NFRA kuleta kituo cha ununuzi wa mahindi hapa kijiji na bei ni nzuri tofauti na ile inayotolewa na wanunuzi wa mitaani wanaonunua kwa Sh.350 hadi 400 kwa kilo moja”aisema Sefu.
Alisema,katika msimu wa kilimo 2023/2024 Chama kilikusanya tani 350 za mahindi kutoka kwa wakulima na katika msimu huu 2024/2025 matarajio ni kukusanya tani 600.
Alisema,kuongezekakwa uzalishaji kumechangiwa sana na watu wengi kulima mahindi baada ya Serikali kurahisisha upatikanaji wa mbolea zinazouzwa kwa bei ya chini ambayo kila mkulima anaimudu.
Mwenyekiti wa Saccos hiyo Elia Tenga,ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya kwani katika kipindi kifupi cha miaka minne ameonyesha kujali matatizo ya wananchi na kuyafanyia kazi.
Alisema,katika kipindi cha miaka minne wakulima wamepata mafanikio makubwa katika shughuli zao kwa kupata soko la uhakika na kulima kwa tija kutokana na uhakika wa kupata pembejeo zinazouzwa kwa bei ya chini ambayo haijawahi kutokea.
“Huko nyuma pembejeo ziliuzwa kwa bei ya juu sana,lakini tangu Rais Samia aingie madarakani kuna tofauti kubwa baada ya kuweka ruzuku kwenye mbolea ambayo imechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mahindi,sasa hivi mkulima ambaye alikuwa halimi sasa amehamasika kulima”alisema Tenga.
Tenga alisema,mbolea za ruzuku zimehamasisha wakulima wengi kujiunga na Chama hicho baada ya kuona mafanikio yaliyopatikana kwa wenzao wanapata soko la uhakika la kuuza mahindi.