TUMEPOTEZA DHANA YA UZALENDO, HATUHESHIMU VIPAJI VYETU ✍️
Sisi sote tupo kwenye anga moja tunaangalia jua moja tofauti yetu ni Nyakati. Mwana Sayansi Albert Einstein alitupa nadharia ya kusafiri ndani ya muda lakini si wote tungeweza kama tungekosa simulizi za waliotutangulia.
Unamkumbuka Ibrahim Jeba ? Kule Jang’ombe walimuita “Faza maiko” . kama alivyojisemea Sam mapangara kuwa “Dunia tunapita”. Kwasasa Jeba amelala kwenye nyumba yake ya milele.
Enzi zake alikuwa Kiungo mwenye dhihaka ya kistaarabu kwa wapinzani, wanasema eti alitoa burudani iliyowafanya walioketi jukwaani waone mpira ni mchezo rahisi mno.
Wanasema Mungu hutoa kila kitu mara mbili ilitupate kuona utukufu wake. Mungu aliyeumba Mbingu na jehannam akaumba mchana na Usiku, akatupa jana na leo . Ametupatia feisal salum “Zanzibar finest” kiungo pekee mwenye vyote walivyokosa wengine kwenye mwili mmoja.
Nani anaesema mpira ni kazi ? tumuoneshe clip za feilasufi akifanya sanaa zote na mpira wake mguuni. Kwa touch zake anatupa fleva ya muziki ambao hautawahi kuimbwa popote kwa lugha ya ulimi hata akiamshwa Michael Jackson. Ni lini tutathamini vipaji Vyetu ?
Ni rahisi kumsikia Mtanzania akisema Yusuph Kagoma ni kiungo wa kizamani. Akimaanisha hatastahili kucheza timu ya taifa. Wanasahau kuwa wachezaji wa aina yake wamekuwa adimu duniani kote. Viungo halisi wa ulinzi ni kama dhahabu kwenye soka la kileo. Labda ni kwasababu Kagoma amezaliwa Kigoma.
Umewahi kujiuliza Kwanini Feisal haimbwi kama wachezaji wa kigeni ? Wakati wengi wao ni kama amewameza wote ndani yake. Fei Toto ni tunu ya Muungano na Definition ya Football” Tanzania.
Medali kadha za ushindi kabatini Class bora back to back. Ila Fei ni yule yule binadamu mwenye aibu ya kusifiwa na wachache walioamua kumpigia makofi.
Mpaka sasa kwenye michuano Ya CHAN wachezaji wa kitanzania wapo katika kiwango bora sana. Ila Ni nani anayewasemea ? Tunasubiri wafanye makosa ili tuanzishe mijadala ya kuwakosoa.
Nionesheni timu nyingine yenye safu nzuri ya kiungo kuliko Tanzania Yangu. Sisi tuna Kagoma, Mudathir na Fei Toto ambao mpaka sasa wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha tunavuka kwenda hatua ya robo fainali. Nyie mna kina nani ?