ISMAILIA:KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United kutoka Botswana hautakuwa mwepesi wanahitaji kujipanga vizuri na kwa umakini mkubwa.
Akizungumzia mchezo huo katika kambi yao iliyoko Ismailia Misri Fadlu amesema wapinzani hao wana sifa ya kucheza kwa kasi, kutumia mbio nyingi na kupigania umiliki wa mpira kwa kiwango cha juu, hivyo wanahitaji umakini mkubwa.
“Gaborone United si timu rahisi. Wana nguvu, wanakimbia sana na wanapigania mpira kila dakika. Tunapaswa kuwa tayari kisaikolojia na kimbinu kukabiliana nao,” amesema Fadlu.
Aliongeza: “Tumepanga mikakati mahsusi kwa mazingira magumu tutakayokutana nayo ugenini, tukijifunza kutokana na changamoto za msimu uliopita, ikiwemo hali ya viwanja na mambo ya nje ya mchezo,” ameongeza.
Katika droo iliyopangwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) Dar es Salaam juzi michezo ya raundi ya kwanza ya hatua ya awali inatarajiwa kupigwa kati ya Septemba 19-21 na marudiano kati ya tarehe 26-28 na michezo ya raundi ya pili ya hatua hiyo itapigwa kati ya Oktoba 17-19 na marudiano wiki moja baadaye.
Ikiwa wekundu wa Msimbazi wataibuka washindi katika mechi hiyo watavaana na mshindi kati ya Simba Bhora ya Msumbiji na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini.
The post Fadlu: Gaborone United sio timu ya kubezwa first appeared on SpotiLEO.