DAR ES SALAAM:KLABU ya Azam FC imemtambulisha rasmi kiungo wa kimataifa wa Mali, Sadio Kanouté, ambaye amesaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo baada ya kuachana na JS Kabylie ya Algeria.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Kanouté aliandika:
“Sura mpya, malengo mapya. Nimejaa shukrani na furaha kujiunga rasmi na Azam. Niko tayari kutoa kila kitu changu kwa ajili ya klabu hii ya ajabu na mashabiki wake wenye shauku. Tufanye historia pamoja!”
Kanouté, mwenye uzoefu mkubwa katika soka la Afrika, alianza kucheza soka la kulipwa akiwa na Stade Malien ya nyumbani kwake Mali, kabla ya kujiunga na Al Ahly Benghazi ya Libya.
Mwaka 2021 alisajiliwa na Simba SC ya Tanzania, ambako aliweka rekodi ya kuwa miongoni mwa viungo bora wa Ligi Kuu na kushiriki michuano mikubwa ya kimataifa. Baada ya misimu mitatu, alihamia JS Kabylie ya Algeria Julai 2024, na kuitumikia hadi mapema 2025.
Sasa, akiwa sehemu ya kikosi cha Azam FC, Kanouté anatarajiwa kuongeza nguvu na uzoefu wa kimataifa katika harakati za klabu hiyo kutafuta mafanikio kwenye Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.
The post Kanoute: Niko tayari kuisaidia Azam FC first appeared on SpotiLEO.