….. OFA IMEKATALIWA. Jana tulilala na neno hili.
Barua za Waarabu zimeendelea kupishana pale Jangwani. Inaingia barua hii, baada ya muda inaingia barua nyingine. Zote zinazungumzia upatikanaji wa Mzize.
Wanachokifanya Yanga SC ni kumtafuta yule mwenye kisu kikali ndio ale nyama. Mimi siamini kama Mzize atacheza Yanga SC msimu ujao. Hili siamini, lakini wanachokifanya Yanga SC ni kuiongezea thamani biashara ya Mzize. Itafika tu timu ambayo itatoa ofa ya maana na itakuwa ngumu ofa hiyo kukataliwa. Uzuri Mzize mwenyewe anazidi kuichonganisha biashara yenyewe. Juzi ametupia mabao mawili katika jezi za Stars.
Ninachoamini iko timu itafikia kiasi ambacho Yanga SC watakipokea. Rais wa Real Madrid Frolentino Perez aliwahi kuwaambia Juventus kuwa hakuna mchezaji asiyeuzwa baada ya kuulizia upatikanaji wa Zidane. Juve ndio walimjibu Perez kwa dharau kuwa Zidane hauzwi.
Baada ya wiki moja Perez kutoa kauli ile, Uwanja wa Santiago Bernabeu ulijaa mashabiki waliokuja kutazama utambulisho wa Zidane. Perez alirudi Juve kikubwa na kutoa fedha ambazo Juve walishindwa kuzikataa. Biashara ya Yanga SC na Mzize itaenda kuisha katika namna hii ya Juve, Zidane na Madrid. Ni ngumu kushikilia bomba hadi mwisho.
Ameandika @abdulmkeyenge1